Na Angela Sebastian
Bukoba : Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 umezindua mradi wa kituo janja cha kusambaza maji wenye thamani ya Sh milioni 11.6, unaolenga kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama katika maeneo ya Shule ya Msingi Ibura, Shule ya Sekondari Elasto Sima pamoja na wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka shule hizo.
Mradi huo unatarajiwa kupunguza adha ya wananchi na wanafunzi kutumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji, huku ukiwa sehemu ya juhudi za kuboresha miundombinu na upatikanaji wa maji katika jamii.
Akizungumza baada ya uzinduzi wa mradi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alimshukuru Rais Dk. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha zinazowezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta ya maji.
Mwang’onda alisema upanuzi wa huduma hiyo utasaidia taasisi hizo mbili za elimu pamoja na wananchi wanaozunguka maeneo hayo kupata huduma ya maji kwa urahisi na uhakika.
“Leo tunashuhudia upanuzi wa huduma ya maji utakaohudumia taasisi zetu hizi mbili, yaani shule ya msingi na sekondari, pamoja na wananchi wengine wanaozunguka maeneo haya. Pia tumezindua mfumo wa kisasa wa upatikanaji wa maji wa malipo ya kabla kupitia njia za kidijitali. Hii inapunguza kutembea mwendo mrefu kulipia huduma hizo,” alisema Mwang’onda.
Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Mhandisi Edmund Deus kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira (BUWASA), ambayo ndiyo inatekeleza mradi huo, alisema mradi huo utawanufaisha wananchi wapatao 788 ambao awali hawakuwa na huduma ya maji safi, salama na ya kutosheleza.
Deus alisema utekelezaji wa mradi huo ni hatua muhimu katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji kwa urahisi, huku ukisaidia kupunguza changamoto ya umbali katika kufuata huduma hiyo pia faida za kituo hicho Cha kidigtal ni kupunguza upotevu wa maji kwani wananchi wakiingiza kadi au sarafu maji yanatoka bila kumwagika chini
Alisema mradi huo pia unaunga mkono kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka 2026 inayosema “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo.”
Kwa mujibu wa BUWASA, mfumo huo wa kisasa wa malipo ya kabla kwa njia za kidijitali unatarajiwa kurahisisha upatikanaji wa huduma ya maji kwa watumiaji, pamoja na kupunguza muda na gharama zinazotumika katika kufuata huduma hiyo.









