NA Angela Sebastian
MULEBA : Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhani Kido, ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026 utakuwa chachu ya kuimarisha maendeleo, amani na mshikamano mkoani humo, huku akiwataka wananchi kuutumia mwenge huo kuibua fursa za kujikwamua kiuchumi.
Kauli hiyo ilitolewa jana wakati wa mapokezi ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa katika Kijiji cha Nyakabango, Wilaya ya Muleba, ambapo Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Mohamed Gombati, alikabidhi mwenge huo kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Steven Ndanki.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Michael Mwang’onda, alizitaka taasisi za manunuzi na Halmashauri zote nane za Kagera kutenga asilimia 30 ya bajeti ya manunuzi kwa ajili ya vikundi vilivyosajiliwa vya vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Alisema hatua hiyo itasaidia makundi hayo kupata fursa za kiuchumi, mikopo na mitaji ya kuanzisha miradi itakayoongeza kipato na kupunguza umaskini.
Aidha, aliwataka wananchi kutumia ujio wa Mwenge wa Uhuru kama fursa ya kuimarisha maendeleo badala ya kuugeuza kuwa chanzo cha migogoro, akisisitiza kuwa changamoto zinapaswa kutatuliwa kwa mazungumzo na ushirikiano.
Kwa upande wake, Kanali Kido alisema Kagera tayari imesajili vikundi 1,455 kati ya 1,200 vilivyolengwa, sawa na asilimia 121, huku vikundi 54 vikiwa vimenufaika na fedha zilizotengwa kupitia manunuzi ya umma.
Alisema Mwenge wa Uhuru utasafiri takribani kilomita 1,230 mkoani Kagera na kutembelea miradi 54 ya maendeleo yenye thamani ya Sh bilioni 23.7.
Kati ya miradi hiyo, 25 itawekewa mawe ya msingi, mitano itafunguliwa, 11 itazinduliwa na 13 itakaguliwa ili kujiridhisha na utekelezaji na manufaa yake kwa wananchi.
Kanali Kido alisema miradi hiyo inagusa sekta muhimu zikiwemo maji, afya, elimu, miundombinu, nishati, uwezeshaji wa vijana na uwekezaji.
Alisema ujumbe wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni “Tanzania ni yetu sote, tushikamane kwa pamoja kuleta maendeleo,” huku ukilenga pia kuhamasisha wananchi kupambana na rushwa, malaria, VVU/UKIMWI na dawa za kulevya, pamoja na kuzingatia lishe bora.
Mkuu huyo wa mkoa aliwahimiza wananchi wa Kagera kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wa Uhuru na kushiriki kikamilifu katika shughuli zake ili kuendeleza mshikamano na kasi ya maendeleo mkoani humo.






