EACOP Yatembelea na Kukagua Mradi wa PS3 Muleba

0


 Na Angela Sebastian 

Muleba : Kituo cha Kusukuma Mafuta Ghafi namba Tatu (PS3) kinachojengwa katika Kijiji cha Kikagate, Kata ya Mubunda, Wilaya ya Muleba mkoani Kagera, kimefikia asilimia 88 ya ujenzi na kinatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Agosti au mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.

Kituo hicho ni sehemu ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), unaounganisha maeneo ya uzalishaji mafuta nchini Uganda na Tanzania.

Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji wa  Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Derick Moshi, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, amesema kukamilika kwa asilimia 88 ya ujenzi wa PS3 ni hatua kubwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Moshi amesema ziara ya wabia na wadau wa mradi huo katika kituo hicho imelenga kujionea maendeleo ya ujenzi na hatua zilizofikiwa pia kuweka msisitizo wa kuhakikisha vituo vyote vya kusukuma mafuta vya mradi huo vikikamilika ifikapo Desemba mwaka hatua itakayosaidia katika kukamilisha maandalizi ya uendeshaji wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki.

Amesema TPDC ikiwa na asilimia 15 ya hisa katika EACOP wameendelea kujifunza kupitia mradi huo, hasa kuhusu ushirikiano wa Serikali na sekta binafsi katika uwekezaji na utekelezaji wa miradi mikubwa yenye umuhimu na ya kimkakati.

"EACOP inamilikiwa na Total Energies yenye asilimia 62, Uganda National Oil Company (UNOC) yenye asilimia 15, Tanzania Petroleum Development Corporation (TPDC) yenye asilimia 15 na CNOOC Limited ya China yenye asilimia 8" ameeleza Moshi.

Meneja wa Kituo cha PS3, Dmitry Malyshev, amesema ujenzi wa kituo hicho ulianza Aprili 2024 na awali ulitarajiwa kukamilika Julai 2026, lakini changamoto za upatikanaji na ucheleweshaji wa malighafi zilisababisha ratiba ya ujenzi kubadilika ambapo kwasasa ujenzi umefikia asilimia 88 na kazi zilizobaki zinaendelea kukamilishwa, ambapo kituo hicho kinatarajiwa kukamilika  kati ya  mwishoni mwezi huu au mwanzoni mwa Septemba mwaka huu.







 

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top