Na Angela Sebastian
Karagwe : Mahakama ya Wilaya ya Karagwe mkoani Kagera imewahukumu mkusanya ushuru wa Kijiji cha Chamchuzi na mfanyabiashara wa samaki miaka mitatu jela au kulipa faini ya shilingi laki tano kila mmoja baada ya kuwakuta na hatia katika mashauri mawili tofauti yanayohusu rushwa.
Mkuu wa Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa mkoa wa Kagera Ismail Bukuku amesema matukio yote mawili yalitokea Juni 20 mwaka huu ambapo katika shauri la kwanza la rushwa namba 15460/2026, lililosikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Charles Ngonyani,mahakama ilimtia hatiani Novart Kahembe Mjungu, ambaye alikuwa mkusanya ushuru wa Kijiji cha Chamchuzi, kwa kosa la rushwa linalohusisha kumpatia fedha Herman Amos Ismael kwa manufaa yake binafsi kiasi cha Shilingi 320,000 ambalo ni shtaka la Rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b)na (2) PCCA Cap 329 [R:E 2023]
Amesema katika shauri jingine namba 15459/2026, lililosikilizwa mbele ya hakimu Elias Bingasira, mahakama ilimtia hatiani tena Herman Amos Ismael, mfanyabiashara wa samaki wa Chamchuzi, kwa kosa la kujipatia Sh82,000 alizokusanya bila kutoa risiti.
Kwa mujibu wa mahakama, washtakiwa wote walishtakiwa kwa kosa la rushwa kinyume na kifungu cha 15(1)(b) na (2) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (PCCA), Sura ya 329, Toleo la Mwaka 2023.
Baada ya kutiwa hatiani, kila mmoja alihukumiwa kulipa faini ya Shl 500,000 au kutumikia kifungo cha miaka mitatu jela endapo wangeshindwa kulipa ambapo wote wawili wawili walilipa faini
Mashauri hayo yaliendeshwa na Mwendesha Mashtaka wa TAKUKURU, Mohamed Kassim Mtambo ambapo, mkuu wa TAKUKURU mkoa Ismail Bukuku amesema hatua hiyo ya mahakama inaonyesha dhamira ya kuendelea kusimamia sheria dhidi ya vitendo vya rushwa.
Amesema Taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na wananchi katika kuzuia na kupambana na rushwa, huku akiwahimiza kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na kuzingatia uwajibikaji katika ukusanyaji na matumizi ya fedha za Umma.


