SMAUJATA Walipongeza HGWT Kupambana na Ukatili, Kusaidia Wasichana Kutimiza Ndoto

0


Na Mwandishi Wetu, Butiama. 

TAASISI  ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) imepongeza juhudi zinazofanywa na  Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania   kwa mchango wake mkubwa katika kupambana na ukatili wa kijinsia na kusaidia watoto wa kike kutimiza ndoto zao  Mkoani Mara. 

Pongezi hizo zimetolewa Julai 10, 2026 na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Utamaduni, Makongamano na Utalii, Hashimu Omary, alipotembelea Kituo cha Nyumba Salama Butiama. Akiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa SMAUJATA kutoka ngazi ya Kanda na Mkoa wa Mara.

Kituo cha Nyumba Salama Butiama kinamilikiwa na shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania. Ambapo limeendelea  kupambana na ukatili wa kijinsia Mkoani Mara kwa kutoa elimu ya ukatili  kwa jamii, makongamano, kutoa msaada kwa wasichana wanaokimbia ukeketaji na  ndoa za utotoni   kwa lengo la kuiwezesha jamii kuachana na vitendo hivyo. 

Akizungumza na wasichana waliopo kituoni hapo, ambao wamepata hifadhi baada ya kukimbia vitendo mbalimbali vya ukatili ikiwemo ukeketaji na ndoa za utotoni kutoka katika familia zao,  Hashimu amewataka kusoma kwa bidii na kusimamia ndoto zao kwani serikali imeweka mazingira bora kwa kila mtoto kupata elimu.

"Nimpongeze Mkurugenzi wa shirika hili, Rhobi Samwelly, kwa maono yake ya kuanzisha Nyumba Salama hii ambayo imekuwa msaada kwenu. Mnapata hifadhi, mnaendelezwa kielimu, na mnapatiwa  mahitaji mbalimbali mkiwa hapa. Someni kwa bidii ili muje kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali na pia muendelee kuwa mabalozi wa kupinga ukatili na kuchochea maendeleo," amesema Hashimu.

Ameongeza kuwa,  SMAUJATA itaendelea kushirikiana na Shirika la Hope, wadau mbalimbali pamoja na Serikali katika kuimarisha mapambano dhidi ya ukatili. Lengo ni kusukuma mbele juhudi za maendeleo na usawa katika jamii kwa manufaa endelevu.

Kwa upande wake, Afisa Mwelimishaji Jamii wa shirika hilo, Emmanuel Good Luck, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Rhobi Samwelly, ameipongeza SMAUJATA kwa kuwatembelea wasichana hao. Amesema, ziara hiyo imewatia moyo wasichana hao na kuwakumbusha kuwa hawako peke yao. 

"Tunawashukuru kwa kuwapa ushauri na kuwatia moyo ili wasijione wapweke. Wametambua kuna watu nyuma yao wanaowaombea kwa Mungu baraka na heri ili wahakikishe wanatimiza ndoto zao, kwani," amesema Good Luck.

Pia, Goodluck amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Mara Kanali Evans Mtambi, kwa kuendelea kukemea vikali vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kuhamasisha mabadiliko chanya kwa  wananchi ili  kuachana na mila potofu na zenye madhara kwa wasichana jambo ambalo  limeendelea kuwa na manufaa katika juhudi za  kutokomeza ukatili mkoani humo.




Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top