Jackline Minja, WMJJWM - Kigoma
Ushirikiano wa jamii, viongozi wa dini, taasisi mbalimbali na vyombo vya dola umetajwa kuwa nguzo muhimu katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kuhatarisha usalama, haki na ustawi wa wanawake, watoto pamoja na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Akizungumza wakati wa Kongamano la Kupinga Ukatili wa Kijinsia lililofanyika katika Ukumbi wa NSSF mkoani Kigoma, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, amesema mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia hayawezi kufanikiwa bila ushirikiano wa Serikali, viongozi wa dini, viongozi wa mila, taasisi mbalimbali na wananchi kwa ujumla, huku akisisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake katika kulinda haki na usalama wa wahanga wa vitendo hivyo.
“Ukatili wa kijinsia si jambo la kawaida wala sehemu ya utamaduni, hivyo hakuna mila, desturi au sababu yoyote inayoweza kuhalalisha kumuumiza, kumdhalilisha au kumnyima mtu haki zake za msingi niwaombe wananchi kuacha kuficha matukio ya ukatili na badala yake kutoa taarifa kwa vyombo husika ili wahusika wachukuliwe hatua za kisheria na kuzuia madhara kuendelea kutokea kwa waathirika wengine”. amesema Naibu Waziri Mahundi
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia pamoja na kuimarisha huduma za ulinzi kwa waathirika huku amekiwataka wazazi na walezi kuzingatia malezi chanya kwa watoto, huku akiwahimiza viongozi wa dini na mila kuendelea kutumia nafasi zao kuelimisha jamii na kukemea vitendo vya ukatili vinavyoathiri maendeleo ya familia na taifa.
"Hakuna atakayefanya vitendo vya ukatili na akabaki bila kuchukuliwa hatua wote watakaobainika kutenda vitendo hivyo watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria, ikiwemo vifungo vya muda mrefu na pale sheria inapotoa nafasi, vifungo vya maisha, ili iwe fundisho kwa wengine basi serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu kila tukio kwa sababu tunataka kujenga jamii ya watu wa mfano.
✍️maendeleo ya jamii









