Serikali Yaweka Vipaumbele Kuendelea Kuimarisha Huduma Za Saratani Nchini

0


Na Mvuda Jaffer, WAF – Dar es Salaam

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mhe. Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema Serikali imeweka vipaumbele vitano vitakavyoimarisha huduma za Neuro-oncology nchini, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kuimarisha huduma za afya za kibingwa na kukabiliana na ongezeko la magonjwa ya ubongo na uti wa mgongo.

Akifungua Kongamano la Kimataifa la Chama cha Madaktari wa Saratani ya Ubongo Afrika , Kusini mwa Jangwa la Sahara (SNOSSA 2026) Julai 13, 2026 jijini Dar es Salaam, Dkt. Nchimbi amesema Serikali itaendelea kuwekeza katika maendeleo ya rasilimali watu kwa kuongeza wataalamu wa magonjwa ya mfumo wa fahamu, upasuaji wa ubongo, radiolojia, saratani na fani nyingine muhimu zinazohusiana na huduma za Neuro-oncology.

Amesema Serikali pia itaendelea kuboresha miundombinu ya afya kwa kuzipatia hospitali za rufaa vifaa vya kisasa vya upasuaji wa ubongo, uchunguzi na huduma za wagonjwa mahututi, sambamba na kuhamasisha matumizi ya mbinu bunifu za kugharamia huduma za afya na kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani ili kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Aidha, Dkt. Nchimbi amesema Serikali itaendeleza matumizi ya teknolojia za kidijitali kupitia mifumo ya usajili wa saratani na rekodi za kielektroniki za wagonjwa ili kuboresha matumizi ya takwimu katika tafiti, ubunifu na utoaji wa huduma bora za afya. 

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kuwawezesha wataalamu wa afya kupata mafunzo na kubadilishana uzoefu kupitia makongamano ya kisayansi yanayochochea maendeleo ya taaluma hiyo.

Amesema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi utaendelea kuimarishwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupanua upatikanaji wa huduma za kibingwa na kuharakisha utekelezaji wa lengo la Huduma za Afya kwa Wote.

Dkt. Nchimbi ameipongeza SNOSSA kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kikanda katika huduma za Neuro-oncology na kueleza kuwa matokeo ya kongamano hilo yatachangia kuboresha kinga, uchunguzi, matibabu na huduma za tiba nafuu kwa wagonjwa wa saratani ya ubongo na uti wa mgongo barani Afrika.

Akihitimisha hotuba yake, Makamu wa Rais amesisitiza kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuongoza juhudi za kuimarisha huduma za Neuro-oncology kupitia uwekezaji endelevu, ushirikiano wa kimataifa na kujenga uwezo wa wataalamu, huku akiwapongeza wataalamu wa afya kwa kujitolea kwao kuhudumia jamii na kuendeleza maendeleo ya sekta ya afya Nchini.









Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top