Na Angela Sebastian
Bukoba : Mkuu wa mkoa wa Kagera Kanali Yahya Ramadhan Kido amewataka viongozi na,watumishi na wataalam wa mkoa huo kuhakikisha wanasimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa ufanisi,weledi,uadilifu na kuzingatia taratibu zote za manunuzi na utaratibu wa mikataba ya inayohusu miradi husika ili raslimali za Umma zitumike kwa ufanisi.
Kanali Kido ametoa maagizo hayo wakati wa warsha maalum iliyoandaliwa na taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU)Mkoa wa Kagera ya kuwajengea uwezo wadau kutoka sekta mbalimbali mkoani humo, juu ya usimamizi na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo amesema katika miradi yote inapaswa kuzingatiwa ubora,muda wa utekelezaji,matumizi sahii ya fedha za Umma na kuhakikisha sheria zinafuatwa kikamilifu.
Aidha amewataka wadau wanaohusika na usimamizi na utekelezaji wa miradi ya mbalimbali ya ujenzi kuhakikisha wanafanya upimaji wa vifaa wanavyotumia katika ujenzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao, sambamba na utatuzi wa haraka wa changamoto zote zinazojitokeza katika usimamizi wa miradi na kufuata sheria.
Ameagiza wakati wa uibuaji wa miradi ya maendeleo na utekelezaji ushilikishe wananchi na isiwepo ucheleweshwaji wa fedha,maafisa masuhuli kuhakikisha mikata yote ya miradi inakaguliwa na mwanasheria wa Halmashauri kabla ya kuanza,kamati za ujenzi na mapokezi zinateuliwa na kujengewa uwezo juu ya miradi na miradi yote itekelezwe pakiwa na mikataba hai.
Naye mkuu wa TAKUKURU mkoa wa Kagera Ismail Bukuku amesema miradi ya maendeleo isiposimamiwa vizuri Taifa haliwezi kusonga mbele,Serikali inatenga kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi na program mbalimbali za kunufaisha wananchi .
"Takukuru imekuwa ikiendesha kampeni mbalilmbali za kupambana na kuzuia na rushwa nchini ili kuviwahi vitendo vya rushwa na kuvizuia visiweze kufanyika,kufanya utafiti na uchambuzi wa vifungu vya kisheria za kitaasisi kwa lengo la kuimalisha mifumo ya utoaji huduma kwa wananchi na kuwaelimisha wananchi ili waichukie rushwa kwani ina madhara makubwa kwa kila mmoja"amesema Bukuku.
Amesema Serikali ya hawamu ya sita inatenga fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo fedha hizo inahitaji uangalizi na usimamizi wa hari ya juu hivyo tunapaswa kudhibiti mianya ya rushwa hasa katika utekelezaji wa miradi husika na kuleta matokeo chanya.












