Rhobi Samwelly Awataka Vijana Kuacha Ulevi, Matumizi ya Madawa ya Kulevya Kulinda Mustakabali Wao

0


Na Mwandishi Wetu, Musoma. 

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojihusisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia Mkoa wa Mara,  Rhobi Samwelly, amewataka vijana nchini kuacha tabia ya kutumia madawa ya kulevya na ulevi kupindukia kwani kufanya hivyo, kunarudisha nyuma mustakabali wa maisha yao.  

Amesema vijana ndio nguvu kazi ya taifa na ndoto zao ziko mikononi mwao. Hivyo, kujihusisha na ulevi na dawa za kulevya ni kujiharibia misingi bora ya kujenga maisha yao wenyewe na  Taifa kwa ujumla.  

Rhobi ametoa wito huo Julai 9, 2026 alipokuwa akizungumza na Musoma News Hub. Mara baada ya kushiriki katika kikao kazi kilichoandaliwa na ICCAO Tanzania katika kutekeleza mradi wa Ulevi Sio Dili katika mkoa wa Mara, Ambapo amebainisha kuwa matumizi ya kupindukia ya pombe na madawa ya kulevya yanaendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wengi kufikia malengo yao. 

"Pombe na dawa za kulevya huharibu afya ya mwili na akili, Vijana wengi hupatwa na magonjwa  Pia husababisha msongo wa mawazo,  na baadhi hata kupoteza uwezo wa kufikiri kwa ufasaha, jambo linalofanya washindwe kusoma au kufanya kazi kwa ufanisi."amesema. 

Amedai kuwa, matumizi hayo hupelekea kutokuwa na nidhamu, uvivu, na kuvunjika kwa mahusiano ndani ya familia na jamii. Wengi pia huingia kwenye makundi mabaya ambayo huwasukuma kufanya vitendo visivyofaa na hatimaye kupoteza heshima mbele ya jamii. 

Kwa mujibu wa Rhobi, taifa linapoteza wataalam na wafanyakazi wengi wenye vipaji kwa sababu ya dawa za kulevya. Amesisitiza kuwa kijana anapotumia muda na fedha zake kununua pombe na madawa, anapoteza fursa ya kujiajiri, kujifunza ujuzi, na kuchangia uzalishaji. 

Ameongeza kuwa,  ulevi kupindukia na madawa ya kulevya ni vyanzo vikuu vya ukatili wa kijinsia, ugomvi na uhalifu miongoni mwa vijana. Huku akisema , shirika lake litaendelea kushirikiana na viongozi wa dini, serikali na wadau mbalimbali kutoa elimu shuleni na mitaani ili kuhakikisha vijana wanapata mwelekeo sahihi na kutimiza ndoto zao.



Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top