👉Yenye thamani ya Bil. 1.4 yakamatwa Kagera
Na Angela Sebastian
SERIKALI imefanikiwa kukamata madini ya aina mbalimbali yaliyokuwa yakitoroshwa na kusafirishwa kinyume cha sheria yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.3 katika matukio 55 yaliyotokea kuanzia Julai 2025 hadi Machi mwaka huu.
Mafanikio hayo yametokana na operesheni zinazoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Wizara ya Madini, vyombo vya dola, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Kamati za Ulinzi na Usalama za Mikoa na Wilaya pamoja na wadau wa sekta ya madini, kwa lengo la kulinda rasilimali za Taifa na kuongeza mapato ya Serikali.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Bukoba (leo) jana wakati wa ziara yake mkoani Kagera, Naibu Waziri wa Madini, Dk. Steven Kiruswa, alisema Serikali imejipanga kuhakikisha madini yote yanayozalishwa nchini yanachangia kikamilifu pato la Taifa kwa kuuzwa na kusafirishwa kwa kufuata sheria.
"Tumefanikiwa kukamata madini yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 3.3 yaliyokuwa yakisafirishwa kinyume cha sheria. Haya ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya Serikali na wadau wote wa sekta ya madini katika kudhibiti utoroshaji wa rasilimali za Taifa," alisema Dk. Kiruswa.
Alisema kati ya matukio hayo 55 ya Julai hadi Machi mwaka huu pia, yapo mawili ambayo yametokea mkoani Kagera katika kipindi cha Juni na Julai mwaka huu ambapo madini yenye thamani ya shilingi bilioni 1.4 yalikamatwa
Katika tukio la Julai 29 mwaka huu majira ya saa tatu usiku katika eneo la Benako wilayani Ngara, Jeshi la Polisi lilikamata gari aina ya Toyota Carina lenye namba T 990 BFW. Baada ya kulifanyia upekuzi, askari walikuta viroba 20 vilivyokuwa na madini ya vito, huku upekuzi uliofuata nyumbani kwa mtuhumiwa ukibaini kiasi kingine cha madini yaliyokuwa yamehifadhiwa.
Dk. Kiruswa alisema madini hayo yalikuwa yanamilikiwa na Petro Marco Kihiga, mwenye leseni ya udalali namba BL 0266LMB/2026 iliyotolewa Mei 25 mwaka huu.
Alieleza kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa amepewa kibali cha kusafirisha gramu 273 za madini kutoka Lindi kwenda Mwanza, lakini alikamatwa akiwa na kilo 627.229 za madini ya vito zenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 10.9. Kodi iliyokuwa inapaswa kulipwa ilikuwa zaidi ya shilingi milioni moja.
"Mtuhumiwa alikiri kosa na kulipa faini kwa mujibu wa sheria," alisema.
Katika tukio jingine lililotokea Julai Mosi mwaka huu, polisi walimkamata mtuhumiwa aliyekuwa akisafiri kwa gari la International Transit (IT) katika eneo la Benako akiwa na madini ya dhahabu yenye uzito wa gramu 4,434.66 na thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 1.3.
Alisema uchunguzi umebaini kuwa dhahabu hiyo ilikuwa ikisafirishwa kutoka Kahama kuelekea mpaka wa Rusumo bila kibali, huku kodi ya Serikali iliyokuwa inastahili kulipwa ikizidi shilingi milioni 125.8.
Aidha, Julai 4 mwaka huu, polisi walimkamata mshirika wa mtuhumiwa huyo akiwa na vipande 20 vya dhahabu vyenye uzito wa gramu 453 na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 144.2, huku kodi iliyokuwa inapaswa kulipwa ikiwa zaidi ya shilingi milioni 12.6.
Dk. Kiruswa alisema watuhumiwa hao wamefikishwa mahakamani na kesi yao inaendelea, huku Serikali ikiacha kutaja majina yao kwa sasa ili kulinda ushahidi.
Aliwataka wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kuzingatia sheria na taratibu zote za biashara hiyo, akionya kuwa yeyote atakayebainika kujihusisha na utoroshaji wa madini atachukuliwa hatua kali za kisheria, ikiwemo kufunguliwa mashitaka ya uhujumu uchumi na utakatishaji wa fedha.
Alisema Wizara ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wadau wote ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa mujibu wa sheria na kulinda rasilimali za Taifa.
Kwa upande wake, mkazi wa Manispaa ya Bukoba, Venanti Simon, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kudhibiti utoroshaji wa madini na kuwataka wachimbaji pamoja na wafanyabiashara kuwa wazalendo kwa kufuata sheria, kupata leseni na vibali halali kabla ya kusafirisha madini.
Alisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mapato ya Serikali yatakayowezesha kuboresha huduma za kijamii ikiwemo ujenzi wa barabara, shule, hospitali na miundombinu mingine muhimu kwa maendeleo ya wananchi.





