Rhobi Samwelly Awataka Wazee wa Mila Kusaidia Mapambano ya Kutokomeza Ukeketaji

0


Na Mwandishi wetu, Serengeti. 

WAZEE  wa Mila Wilayani Serengeti Mkoani Mara, wamehimizwa kuendelea kuunga mkono  juhudi  za kutokomeza ukeketaji na ndoa za utotoni,  hatua ambayo itawezesha watoto wa kike kusoma na kutimiza ndoto zao. 

Rhobi Samwelly Mkurugnzi wa Hope for Girls and Women in Tanzania ameyasema hayo julai 27, 2026, wakati wa zoezi la utoaji wa elimu na usambazaji wa Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa kutokomeza ukeketaji wa 2025/26-2029/30 lililofanyika katika kata za Rung'abure, Nyansurura na Kata ya Kibanchabancha  Wilayani Serengeti Mkoani Mara. 

Mkakati huo unasambazwa na Timu  maalum kutoka  Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na makundi Maalum pamoja na wadau katika mikoa ambayo inafanya ukeketaji.  Lengo la Mkakati huo    ni kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini Tanzania kwa  asilimia 50, kutoka asilimia nane  mwaka 2024/2025 , hadi asilimia nne, ifikapo mwaka 2029/30. 

Rhobi amesema kuwa, Wazee wa Mila  wanawajibu wa kuhakikisha wanakemea mila hiyo kwa nguvu zote, kutokana na madhara ya mila hiyo ikiwemo  kurudisha maendeleo ya wasichana kielimu, kuwaathiri kiafya, na kukwamisha ndoto zao  na jamii kwa ujumla. 

Amesema,  matarajio ya mpango mkakati huo ni kuhakikisha ifikapo 2030 utekelezaji wake unaleta matokeo ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ukeketaji, jamii kuachana na mila zenye madhara, utekelezaji mzuri wa sheria, ushirikiano wa kisekta na matumizi bora ya takwimu na tafiti.  

"Wazee wa Mila ni Wadau muhimu katika mapambano haya, endeleeni kushirikiana na serikali kukemea mila hii. Himizeni watoto wasome kwa faida yao na Taifa letu, lakini pia jamii nzima ioneshe ushirikiano madhubuti katika kuunga mkono kufanikisha Mkakati huu ufanikiwe ipasavyo."amesema Rhobi. 

Rhoda Samson ni Mkazi wa Kata ya Rung'abure amesema kuwa, mkakati huo ni dira nzuri ya kutokomeza ukeketaji,  ameomba elimu kuhusu Mkakati huo, izidi kutolewa kwa wananchi waufahamu zaidi na kuutekeleza kikamilifu kwa kuachana na ukeketaji na kuwafanya watoto wa kike wawe salama. 

Naye Suleman  Bishagazi Mhamasishaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amesema Mkakati huo umeshirikisha wadau wote na kwamba umempa  kila Mdau nafasi ya  kuwajibika kuhakikisha ukeketaji unakwisha. 

Bishagazi amesema, kila mwananchi  anawajibu wa kuhakikisha mtoto wa kike na wanamke wanalindwa dhidi ya ukeketaji, kwani mila hiyo ni kinyume cha haki za binadamu na sheria za nchi. Hivyo, serikali lazima iendelee kuchukua hatua za kisheria kwa wote wanaojihusisha na mila hiyo.







Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top