Na Emmanuel Chibasa
Ni jambo la kawaida ukifika katika baadhi ya maeneo ya
fukwe na mialo ya Ziwa Victoria nyakati za jioni na kukuta wavuvi wamekusanyika kwa makundi, wakipakia nyavu zao na vitendea kazi vingingine kwenye
mitumbwi kabla ya kuanza safari ya usiku kutafuta samaki na dagaa.
Baadhi yao huonekana wamevaa life jackets huku wengine wakiwa hawajavaa lakini kwa wengi, hilo si chaguo la uhakika wa usalama ni chaguo la kuendelea kuishi kama anavyoeleza Josiah Sabato
“Tunavaa hizi life jacket lakini
sisi tunaziona hazina ubora kabisa sijui kwa kwa sababu ya bei tunayonunua ni
ya kiwango cha chini au sehemu
zinapotengenezwa wanaengeneza chini ya kiwango labda viongozi huko ndio watuambie Kwa Nini zipo hivi sababu ikitokea mtu amezama itamsaidia kwa muda mfupi sana tofauti na watu huko nje wanavyouchukulia ” Anasema Josia
Lakini licha ya hofu hiyo,
hakuna anayebaki nyumbani. Kila mtu ana sababu moja inayofanana.
“Tunajua watu wanazama lakini tukikaa nyumbani familia itakula nini? Huku sisi ndio sehemu tunapata pesa ya chakula, ada za
watoto na mahitaji mengine"
Licha ya changamoto hizo lakini hakuna anayebaki nyumbani kama ilivyo kwa Josia, ambaye anaeleza wazi kwamba Ziwa Victoria sio tu ni sehemu ya kupata mazao ya samaki, bali pia ni sehemu ya kujipatia riziki katika kukuza uchumi binafsi na taifa kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Wizara ya
Mifugo na Uvuvi, Sekta ya Uvuvi imeendelea kuwa nguzo muhimu katika uchumi wa
taifa, ikichangia asilimia 1.6 ya Pato la Taifa (GDP) mwaka 2024 na kukua kwa
asilimia 2.3.
Sekta hiyo pia inakadiriwa
kunufaisha zaidi ya Watanzania milioni 6 katika mnyororo wa thamani, kuanzia
uvuvi, usindikaji, biashara hadi usafirishaji.
Hata hivyo nyuma ya takwimu hizi za mafanikio ya kiuchumi, kuna simulizi tofauti kabisa katika mwambao wa Ziwa Victoria simulizi ya maisha yanayoishi hatarini kila siku.
Maisha ya Hatari Ziwani
Adam
Maingu (58), mkazi wa Nyakato Mlimani Manispaa ya Musoma anajishughulisha na
uvuvi wa dagaa katika Ziwa Victoria, anasema kazi hiyo imekuwa sehemu ya maisha
yake ya kila siku. Anaeleza kuwa kwa wiki huenda ziwani mara sita au hata saba
kutegemeana na hali ya hewa na mara nyingine hurudi mikono mitupu lakini hana
namna nyingine ya kujipatia kipato cha kuendesha maisha ya familia yake.
Anasema changamoto kubwa
inayomkabili katika kazi yake hiyo ni ukosefu wa life jacket kutokana na gharama
kuwa juu, hali inayowafanya baadhi ya wavuvi pia kutegemea vifaa vilivyopo
kwenye mtumbwi ambavyo mara nyingi havitoshi.
Anakumbuka tukio la hatari siku
moja walipokutana na upepo mkali na mawimbi makubwa yaliyotokea ghafla usiku
wakiwa ziwani, ambapo mtumbwi wao ulianza kujaa maji kidogo kidogo na
walilazimika kupambana kwa muda mrefu kabla ya kufika salama ufukweni.
“ licha ya hatari hizo, uvuvi bado ni tegemeo lake kuu la maisha kwani ndiyo unaomwezesha kuhudumia familia, kulipa ada za watoto na kugharamia mahitaji ya kila siku, hivyo anaendelea kufanya kazi hiyo huku akichukua tahadhari kadiri iwezekanavyo.’Amesema Adam
Ajali Zinavyo badilisha
Maisha
Idd
Magere (42), mkazi wa Machinjioni kata ya Rwamlimi Manispaa ya Musoma na mvuvi
katika Ziwa Victoria, anasimulia tukio la hatari lililobadilisha mtazamo wake
kuhusu usalama majini. Anasema akiwa pamoja na wenzake ziwani hali ya hewa
ilibadilika ghafla, upepo mkali ukaanza kuvuma na mawimbi makubwa. Katika hali
hiyo, mtumbwi mmoja uliokuwa karibu yao ulipigwa na mawimbi na kupinduka, na
waliokuwa ndani yake walijikuta wakipambana kuogelea lakini si wote waliweza
kujiokoa.
Anasema eneo la ajali
lilikuwa mbali na nchi kavu na hakukuwa na boti ya uokoaji karibu jambo
lililofanya juhudi za msaada kuwa ngumu zaidi. Waliopata ajali hawakuwa wamevaa
life jacket hivyo walichoka haraka walipojaribu kuogelea. Anasema wao
walijaribu kusaidia kwa kutumia mitumbwi wao, lakini uwezo wake ulikuwa mdogo
na kuchelewa kuwafika kuliathiri uokoaji.
“Tukio hilo lilinifundisha kubadilika nikiwa majini, siku hizi nangalia hali ya hewa kabla ya safari na pale ninapoona dalili za upepo mkali au mvua huahirisha safari licha ya changamoto za kipato na kutumia mtumbwi wa kasia, kuchukua tahadhari na kutumia life jackets pale inapowezekana ni hatua muhimu ya kuokoa maisha ingawa hizi life jacket tunazovaa hata ukizama nusu saa tu unaenda nayo chini.’Ameongeza Idd
Uelewa na Tabia za Wavuvi
Damas
Leonard mvuvi katika eneo la Mwisenge na mkazi wa Kamnyonge Manispaa ya Musoma anasema
wavuvi wengi katika mwambao wa Ziwa Victoria hutegemea zaidi uzoefu wao wa muda
mrefu kuliko elimu rasmi ya usalama majini. Anasema hali hiyo imekuwa
changamoto kwa sababu uzoefu pekee hauwezi kutabiri mabadiliko ya ghafla ya
hali ya hewa ziwani jambo linaloweka maisha ya wavuvi hatarini hasa wanapoingia
majini bila tahadhari za mwongozo wa kitaalamu.
Naye Zakayo Mauma ambaye pia ni mvuni na mkazi wa mkinyerero manispaa ya Musoma akieleza kuwa, licha ya taarifa za hali ya hewa kupatikana kupitia vyombo vya habari, bado baadhi ya wavuvi huzipuuza na kuendelea na safari zao kama kawaida. Anasema tabia hiyo inachochewa na uhitaji wa kipato cha haraka, lakini imekuwa ikisababisha ajali zinazoweza kuzuilika, hasa pale hali ya hewa inapobadilika ghafla wakati wavuvi wakiwa tayari ziwani.
Gharama ya Vitendea Kazi na Hali ya Usalama
Bahati
Kabasa mmiliki wa mtumbwi wa mvuvi wa dagaa katika eneo la Mwisenge Manispaa ya
Musoma, anasema changamoto kubwa inayowakabili wamiliki wa mitumbwi na wavuvi
ni bei kubwa na upatikanaji mdogo wa life jackets zenye ubora.
“Hali
ya upatikanaji wa samaki na dagaa kwa sasa imepungua sana na inatulazimu wavuvi wetu kwenda umbali mrefu zaidi ziwani kutafuta riziki lakini hata hivyo mavuno bado
ni madogo na muda mwingine wanakosa kabisa lakini unakuta tunatumia gharama
kubwa za uendeshaji hali inayopelekea kushindwa kumudu kununua life jackets zenye ubora.” Amesema Bahati
Anasema kutokana na kipato kupungua wavuvi wengi pamoja na wamiliki wa mitumbwi hushindwa kumudu kununua life jackets zenye ubora wa juu.
Bahati anasema baadhi ya life jackets
zinazopatikana sokoni huuzwa kati ya shilingi 20,000 hadi 25,000 lakini hazina
uwezo wa kutosha wa kuokoa maisha ambapo ametoa wito kwa serikali kuangalia
ubora wa bidhaa hizo katika maduka lakini pia kupunguza gharama au kutoa ruzuku, akisema endapo life jackets
bora zingepatikana kwa bei ya chini wavuvi wengi wangeweza
kumudu na kuongeza usalama wao majini.
Robinson
Wangaso ni mjumbe wa kamati ya maafa na habari wa Tanzania Red Cross Society
mkoa wa Mara, anasema sababu kuu zinazochangia matukio ya watu kuzama katika
Ziwa Victoria ni pamoja na kutotumia vifaa vya kuokoa maisha kama life jackets,
matumizi ya vyombo visivyo salama au vilivyochakaa, pamoja na kupakia abiria na
mizigo kupita uwezo wa vyombo hivyo. Pia anasema baadhi ya wavuvi na wasafiri
huendelea na safari hata wakati wa upepo mkali na mawimbi makubwa jambo
linaloongeza hatari ya ajali zinazoweza kuzuilika.
Anasema makundi yaliyo katika
hatari zaidi ni wavuvi wadogo, wasafiri wa kila siku wanaotumia usafiri wa
majini, watoto wanaoishi karibu na fukwe za Ziwa Victoria pamoja na wananchi
wasiokuwa na ujuzi wa kuogelea. Hali hii inaonyesha kuwa changamoto ya kuzama
si ya kundi moja pekee, bali ni ya kijamii na kiuchumi inayogusa maisha ya watu
wengi, hivyo elimu ya usalama majini na matumizi ya vifaa vya kujikinga ni
muhimu zaidi.
“Tanzania Red Cross Society
imekuwa ikiendesha kampeni za uhamasishaji katika mwambao wa Ziwa Victoria,
ikisisitiza matumizi ya life jackets, kuzingatia utabiri wa hali ya hewa kabla
ya safari na kufuata taratibu za usalama majini. Pia tumekuwa tukitoa mafunzo
ya huduma ya kwanza na mbinu za msingi za uokoaji kwa jamii ili kuongeza uwezo
wa kutoa msaada wa haraka pindi ajali zinapotokea.” Amesema Wangaso
Ameongeza kuwa mbali na kuendesha kampeni hizo lakini bado kuna changamoto upungufu wa vifaa vya kisasa vya uokoaji kama boti za uokoaji, vifaa vya mawasiliano na huduma ya kwanza, pamoja na umbali wa baadhi ya maeneo ya ajali unaochelewesha uokoaji ambapo anasisitiza kuwa suluhisho linahitaji ushirikiano wa serikali, Red Cross na jamii kwa pamoja ikiwemo utekelezaji wa sheria za usalama majini, ukaguzi wa vyombo vya usafiri na kuongeza vituo vya uokoaji katika maeneo hatarishi.
Kwa
mujibu wa Shirika la Chakula na Kilimo la
Umoja wa Mataifa (FAO),
zaidi ya wavuvi 32,000
hupoteza maisha kila mwaka duniani kutokana na ajali mbalimbali zinazotokea
majini. Shirika hilo linaeleza kuwa idadi hiyo huenda ikawa ndogo kuliko hali
halisi kutokana na changamoto za kuripoti vifo vinavyotokea baharini na
maziwani.
FAO inaeleza kuwa karibu watu milioni 60 duniani wanajishughulisha na sekta ya uvuvi na ufugaji wa samaki, huku wengi wao wakiwa katika nchi zenye kipato cha chini na cha kati. Wanawake wanakadiriwa kuunda asilimia 21 ya nguvu kazi katika sekta hiyo, na zaidi ya asilimia 40 ya samaki wanaovuliwa duniani hutokana na uvuvi mdogo. Pamoja na mchango huo mkubwa katika usalama wa chakula na uchumi, hatari ya kuzama majini imeendelea kuwa moja ya vihatarishi vikubwa vinavyowakabili wavuvi katika shughuli zao za kila siku.
Pengo la Sera na Uhalisia
Mujura
Maingu ni Afisa mradi wa Lake Victoria Drowning Prevention Project (LVDPP) mkoa
wa Mara unaotekelezwa na shirika la Environmental Management and Economic
Development Organization (EMEDO).
Amesema ajali nyingi za
majini hazizungumzwi sana kwa sababu ni suala la kisera na kwa muda mrefu
hakuna sera mahususi inayolenga moja kwa moja usalama wa maisha ya watu majini.
Anasema hata katika Sera ya Uvuvi, suala la usalama wa watumiaji bado halipewi
uzito wa kutosha.
Amesema Sera zilizopo
zinajikita zaidi kwenye masuala ya uzalishaji, mapato, usimamizi wa rasilimali
za uvuvi na tozo, lakini hazijazingatia kwa kina usalama wa watu wanaotumia
maji kama sehemu ya maisha yao ya kila siku. Hii inaleta pengo kubwa kati ya
uhalisia na mipango ya kitaifa.
Ameeleza kuwa utafiti
unaonyesha makundi yaliyo hatarini zaidi ni wavuvi wanaokwenda ziwani kuvua,
wasafiri wanaotumia usafiri wa majini, pamoja na wananchi wanaotumia ziwa kwa
shughuli za kawaida kama kufua au kuoga, wakiwemo watoto na wanawake.
“ili kupunguza ajali za
majini hatua ya kwanza ni elimu ya uelewa kwa jamii, kwa sababu watu wengi
wamekuwa wakichukulia hatari za ziwani kama jambo la kawaida licha ya vifo
vinavyoendelea kutokea.
Kupitia mradi wetu tumefanikiwa
kuboresha mwitikio wa jamii katika kutoa taarifa za ajali ambapo awali wananchi
walikuwa wazito kutoa taarifa, lakini sasa taarifa hutolewa haraka kwa viongozi
na timu za uokoaji.
Changamoto nyingine
tulioibaini katika utafiti wetu wavuvi walieleza kuwa mitumbwi inayotumika sasa
haina uwezo wa kuelea vizuri kama ilivyokuwa zamani kutokana na na aina za mbao
wanazotumia kutengeneza, tofauti na mitumbwi ya zamani iliyokuwa na uwezo wa
kumsaidia mtu kubaki juu ya maji hata baada ya ajali kwa sasa mitumbwi mingi
hutengenezwa kwa mbao duni na wakati mwingine inapozama huishia kuzama kabisa
hadi kwenye tope jambo linaloongeza hatari ya vifo.” Amesema Maingu
Ameongeza kuwa kupitia mradi
huo wamehamasisha matumizi ya life jackets kama suluhisho la haraka pamoja na ukarabati wa vyombo vya usafiri
majini ili kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika lakini hata hivyo anasema
changamoto kubwa bado ni gharama ya life jackets, ambapo sheria inamtaka
mmiliki wa chombo kuwanunulia wafanyakazi wake, lakini wamiliki wengi wanasema
kipato ni kidogo na hawawezi kumudu.
Aidha amesema mradi huo
umetengeneza life jackets 500 na kuzipunguza bei kutokana na kutengenezwa kwa
ruzuku kutoka shilingi 70,000 hadi 40,000, lakini bado wavuvi wengi wanashindwa
kununua na badala yake huchagua zile za bei nafuu ambazo hazina uwezo wa kuokoa
maisha kwa muda mrefu.
Taasisi ya Environmental Management and Economic Development Organization (EMEDO) kwa kushirikiana na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO),zimekua zikishirikiana kutekeleza juhudi za kuongeza uelewa wa jamii na kujenga uwezo wa wananchi katika kuzuia vifo vinavyotokana na ajali za kuzama katika Ziwa Victoria.
Ushirikiano huo unalenga kuimarisha elimu ya usalama majini na kukuza ujuzi utakaosaidia kuokoa maisha ya wavuvi na watumiaji wengine wa ziwa hilo lenye ukubwa wa zaidi ya kilomita za mraba 68,000, na kutegemewa na wavuvi zaidi ya 100,000 kama chanzo kikuu cha maisha yao. Hata hivyo, FAO linaonya kuwa wavuvi pamoja na jamii zinazozunguka ziwa hilo wanaendelea kuwa katika hatari kubwa ya kupoteza maisha kutokana na ajali za kuzama majini
Je Upi Mkakati wa Serikali katika
Huduma za Utafutaji na Uokozi
Wakati wavuvi na wadau wa
maendeleo wakieleza changangamo za usalama majini katika Ziwa Victoria Serikali kwa upande wake imesema
itaendelea kuwekeza katika sekta ya usafiri wa majini na kuimarisha huduma za
utafutaji na uokozi kama sehemu ya juhudi za kulinda maisha ya wananchi,
kuongeza usalama wa usafiri wa majini na kuchochea ukuaji wa uchumi wa buluu.
Akizungumza tarehe 25 Juni
2026 wakati alipotembelea Boti ya Utafutaji na Uokozi ya Shirika la Uwakala wa
Meli Tanzania (TASAC) katika Bandari ya Kigoma, ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho
ya 16 ya Siku ya Mabaharia Duniani, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa
alisema serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu, vifaa na vyombo vya
kisasa vya uokozi ili kuboresha usalama wa watu wanaotumia usafiri wa majini.
Prof. Mbarawa alisema TASAC
imeendelea kutekeleza maelekezo ya serikali kwa kusimamia ununuzi wa boti za
kisasa za utafutaji na uokozi zilizogharimu zaidi ya shilingi bilioni mbili
hatua iliyoongeza uwezo wa kukabiliana na dharura katika maeneo ya maziwa na
bahari huku akisisitiza kuwa, kuongezeka kwa shughuli za usafiri na biashara
kupitia maji kunahitaji mifumo imara ya uokoaji na usimamizi wa usalama ili
kupunguza ajali na kulinda maisha ya wananchi, huku uwekezaji huo ukiwa sehemu
ya mkakati mpana wa kuimarisha uchumi wa buluu nchini.
Lembris Machungwa ni Afisa Uvuvi wa Manispaa ya Musoma anasema moja ya changamoto kubwa inayochangia ajali za majini ni baadhi ya wavuvi kutovaa life jackets licha ya kufahamu umuhimu wake.
Anasema hali
hiyo inatokana na mazoea ya muda mrefu, kwani kwa miaka mingi wavuvi walikuwa
wakifanya shughuli zao bila kutumia vifaa hivyo vya usalama.
“Kutokana
na utamaduni huo imekuwa vigumu kwa baadhi yao kubadili tabia na kuanza kuvaa
life jackets kila wanapoingia ziwani na pia kiwango kidogo cha uelewa kuhusu usalama
majini na umuhimu wa kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa kimeendelea
kuchangia baadhi ya wavuvi kuvunja taratibu za usalama, hivyo kuongeza hatari
ya ajali.” Amesema Machungwa
Machungwa anasema Ofisi ya Uvuvi ya
Manispaa ya Musoma imekuwa ikiendesha vikao vya kila robo mwaka na wadau wa
sekta ya uvuvi, ambapo pamoja na masuala ya maendeleo ya sekta hiyo, ajenda za
usalama majini hupewa kipaumbele kwa kutoa elimu na kuhamasisha matumizi ya
vifaa vya kujikinga.
Anatoa wito kwa wavuvi
kuhakikisha wanavaa life jackets kila wanapoingia ziwani, kutumia vyombo
vinavyokidhi viwango vya usalama na kuzingatia taarifa za hali ya hewa kabla ya
safari, akisisitiza kuwa kuchukua tahadhari ni hatua muhimu ya kulinda maisha
na kupunguza ajali zinazoweza kuzuilika.











