Na Mwandishi wetu, Mara.
WANANCHI wa Wilaya za Tarime na Serengeti Mkoani Mara wamelipongeza Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) kwa mchango wake mkubwa wa kuokoa na kuwawezesha wasichana wengi kutimiza ndoto zao, sambamba na kuongeza uelewa wa jamii juu ya madhara ya ukatili wa kijinsia.
Wameyasema hayo Julai 29, 2026 wakati wa kilele cha kampeni ya utoaji elimu na usambazaji wa Mkakati wa Taifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji 2025/26-2029/30, iliyofanyika Nyamongo Wilaya ya Tarime Mkoa wa Mara.
Wankuru Marwa, mkazi wa Rung'abure Wilaya ya Serengeti, aliyehudhuria katika kilele hicho, amesema shirika hilo limekuwa mkombozi kwa wasichana wengi katika Wilaya hiyo ambao ndoto zao zingefifia na kupotea.
“Wasichana ambao walikuwa katika hatari ya kukeketwa ili waozeshwe na wazazi wao, wameendelezwa kielimu. Uwepo wa shirika hili umekuwa msaada mkubwa. Naiomba Serikali ichukue hatua kali kwa wazazi wanaokiuka sheria na kutaka kuwakeketa watoto wao,” amesema Wankuru.
Rhoda Chacha, mkazi wa Kata ya Kemambo Wilaya ya Tarime, amesema HGWT imechangia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwelewa kwa wananchi kupitia mikutano ya hadhara na makongamano mbalimbali vijijini.
Anitha Nyangi, mkazi wa Itiryo Wilaya ya Tarime, ambaye zamani alikuwa mkeketaji. Amesema kuwa "Nilielimishwa madhara ya ukeketaji, nikaambiwa ni kosa kisheria, nikaacha. Kwa sasa mimi ni balozi wa kuelimisha wananchi wasikekete watoto wa kike, bali wawasomeshe kwa faida yao siku za usoni” amesema Nyangi.
“Nilikuwa nataka kumkeketa binti yangu ili aolewe. Lakini alikimbia na kwenda nyumba salama Hope for Gorls. Leo hii anasoma chuo kikuu mwaka wa tatu, anasoma Uhasibu. Nina imani atatimiza ndoto zake ambazo mimi mwenyewe nilitaka kuzikwamisha,” amesema Bhoke Mwita.
Boniphace Samson Mkazi wa Nkende Wilaya ya Serengeti amesema ushirikiano kati ya Serikali, viongozi wa jadi na mashirika kama HGWT ndio ufunguo wa kuhakikisha wasichana wa Mara wanapata fursa sawa ya kusoma na kutimiza ndoto zao bila hofu ya ukatili.
Rhobi Samwelly, Mkurugenzi wa Shirika hilo, amesema kuwa shirika analoliongoza litaendelea kushirikiana na serikali na Wadau kuhakikisha linatoa elimu kwa wananchi kuwezesha kufanikisha kutokomeza ukeketaji mkoani humo.
Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele, akizungumza katika kilele hicho, ameyashukuru mashirika ambayo yanapambana na ukatili hatua ambayo amesema yamezidi kustawisha maendeleo ya watoto wa kike. Huku akiomba jamii kuachana na mila mbaya.
Mkakati wa Taifa uliosambazwa na timu maalum kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na wadau, umewafikia takribani wananchi 10,000, katika mikoa yote inayofanya ukeketaji. Unalenga kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini kwa asilimia 50. Kutoka asilimia 8 mwaka 2024/2025 hadi asilimia 4 ifikapo mwaka 2030.
![]() |







