Zaidi ya wakulima 200 wa zao la pamba kutoka vijiji vya Mwahalanga, Bukama, Mwabakima, Jogoya na Jilelabalimi vilivyopo katika Wilaya ya Igunga, Mkoa wa Tabora, wamefungua akaunti za benki na kusajili laini za simu ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya kupokea malipo ya mazao yao kwa njia ya kidijitali, hatua inayolenga kuongeza uwazi, usalama na uharaka wa malipo.
Wakulima hao wamefungua akaunti kupitia Benki ya NMB pamoja na kusajili laini kupitia Mtandao wa simu wa Mixx by Yas, hatua ambayo itawawezesha kupokea fedha zao kwa urahisi kupitia mifumo ya benki na simu za mkononi.
Ufunguzi wa akaunti hizo na usajili wa laini za simu unatekelezwa kufuatia maelekezo ya waraka wa Mrajis wa Vyama vya Ushirika unaozitaka AMCOS za wakulima wa pamba kuhakikisha malipo ya wakulima yanafanyika kupitia akaunti za benki na huduma za fedha kwa njia ya simu, badala ya kutumia mfumo wa malipo ya fedha taslimu (cash). Lengo la hatua hiyo ni kuongeza uwazi, usalama wa fedha za wakulima, kurahisisha ufuatiliaji wa malipo na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza katika matumizi ya fedha taslimu.
Akizungumza wakati wa zoezi hilo, Mrajis Msaidizi (Uhamasishaji) Ibrahim Kadudu amesema kuwa mwitikio wa wakulima umekuwa mkubwa baada ya kupata elimu kuhusu umuhimu wa kutumia huduma rasmi za kifedha katika malipo ya mazao yao.
Alieleza kuwa matumizi ya akaunti za benki na huduma za kifedha za simu yataondoa changamoto zilizokuwa zikijitokeza katika mfumo wa malipo ya fedha taslimu na kuhakikisha wakulima wanapata fedha zao kwa wakati, kwa usalama na kwa uwazi zaidi.
Aidha,ameeleza kuwa kuwa zoezi hilo ni sehemu ya utekelezaji wa maelekezo ya Serikali ya kuimarisha usimamizi wa malipo ya mazao kupitia mifumo rasmi ya kifedha, huku ikihamasisha wakulima kujiunga na huduma za benki na fedha za simu.
Sambamba na hilo TCDC, imewasisitiza wakulima wote wa zao la pamba nchini kufungua akaunti za benki na kusajili laini za simu zinazotumika katika huduma za kifedha, ili kuwezesha malipo yote ya mazao yao kupita katika mifumo ya benki na simu za mkononi badala ya malipo ya fedha taslimu.










