Na Ghati Msamba
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh Dk. Samia Suluhu Hassan na Rais wa Jamhuri ya Singapore, Mhe. Tharman Shanmugaratnam, wameshuhudia utiaji saini wa Hati ya Makubaliano kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Singapore kuhusu Uendelezaji wa Ujuzi na Rasilimali Watu.
Makubaliano hayo yanakusudia kuimarisha mafunzo ya kitaalamu, ujenzi wa uwezo pamoja na kubadilishana uzoefu katika maendeleo ya rasilimali watu ili kuongeza ufanisi katika utendaji wa taasisi za umma na sekta nyingine za maendeleo.
Hati hiyo ilisainiwa Juni 9, 2026 katika Ikulu ya Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa upande wa Tanzania, na Waziri wa Nchi wa Wizara ya Mambo ya Nje, Familia na Maendeleo ya Jamii wa Singapore, Mhe. Zhulkarnain Abdul Rahim kwa upande wa Singapore.
Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Rais Dk. Samia amesema ushirikiano huo ni hatua muhimu katika kuendeleza rasilimali watu na kuongeza uwezo wa watumishi kupitia mafunzo na programu za kubadilishana uzoefu.
Kwa upande wake, Rais Tharman Shanmugaratnam amesema makubaliano hayo yataimarisha uhusiano wa kirafiki na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Singapore, hususan katika maeneo ya maendeleo ya watu, elimu na ujenzi wa uwezo wa taasisi.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kufungua fursa zaidi za mafunzo, uhamishaji wa maarifa na KUIMARISHA uwezo wa rasilimali watu Kwa manufaa ya mataifa yote mawili.






