WANANCHI wanaoishi kandokando ya Ziwa Victoria wilayani Rorya mkoani Mara wameiomba Serikali kuingilia kati vitendo vya uvamizi vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya watu kutoka nchi jirani za Kenya na Uganda, wanaofahamika kwa jina la "Mama Lao".
Hayo yalibainishwa katika mkutano wa hadhara kilichofanyika katika kata ya Kiyang'ombe,
Mgasa chacha, alisema wamekuwa wakikumbwa na matukio ya kuvamiwa wakiwa ziwani, kuporwa samaki, mitumbwi pamoja na mali nyingine wanazomiliki.
Wananchi hao walidai kuwa baadhi ya matukio hayo yamekuwa yakihusisha ukatili mkubwa, ambapo baadhi ya wavuvi wamejeruhiwa na wengine kupoteza maisha baada ya kushambuliwa na kufungiwa jiwe na baadae kutupwa ziwani.
"Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kulinda usalama wetu na mali zetu, wavuvi wengi wanaishi kwa kutegemea shughuli za uvuvi, lakini sasa wanahofia kwenda ziwani kutokana na matukio haya," amesema Mgasa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Patric Chandi, amesema ni muhimu kwa vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa shughuli za uvuvi kuchukua hatua madhubuti za kukabiliana na vitendo hivyo na kulinda maslahi ya wananchi wa maeneo ya mwambao wa Ziwa Victoria.


