Wananchi Musoma Walalamikia Mitungi ya Gesi Kupungua Ujazo, EWURA Kanda ya Ziwa Yatoa Tahadhari

0


Na Emmanuel Chibasa

Jane Magembe mkazi wa Mwisenge Manispaa ya Musoma, alikuwa ameamua kuachana na matumizi ya mkaa na kuhamia gesi ya kupikia ili kupunguza gharama na kulinda afya ya familia yake. Hata hivyo  amejikuta akijiuliza swali moja kubwa kwamba kwa nini gesi anayoinunua wakati mwingine inawahi kuisha na haidumu kama ilivyokuwa awali?

"Nilikuwa naagiza gesi kwa boda boda kama kawaida lakini kuna wakati mtungi haukai hata mwezi mmoja umeisha. Nilipojaribu kuuliza wauzaji madukani walidai hata wao hawaelewi sababu wakisema hata wao wanachukua kutoka kwa wasambazaji  ikiwa hivyo," Anasema Jane.

Malalamiko ya Jane si ya pekee. Monica Edward wa eneo la Mtakuja naye anasema watumiaji wa gesi kupikia wamekuwa wakikumbana na hali hiyo kwa kununua bidhaa ambayo hawawezi kuthibitisha ujazo wake kwa macho na maduka mengi wanatoa huduma hiyo bila ya mizani.

"Changamoto ni kwamba unanunua au unapoenda kujaza mtungi wa gesi lakini huwezi kujua kama umejazwa kikamilifu. Maduka mengi ya mtaani hayana mizani. Bei za gesi zimepanda lakini bado tunaamua kutumia gesi inasikitisha kuona wakati mwingine gesi inaisha haraka bila sababu za msingi. Serikali inapaswa kufanya uchunguzi ili tujue nani anatuchakachua," Anasema Monica.

Kwa Daniel Arobogast, suluhisho ni kuweka mfumo wa lazima wa kupima mitungi yote ya gesi mbele ya mteja.

"Kama EWURA wamegundua changamoto hii ni muhimu wachukue hatua haraka. Kila mfanyabiashara wa gesi anatakiwa kuwa na mzani wa kupima mtungi wakati wa kuuza au kujaza. Watakaokiuka utaratibu huo wachukuliwe hatua kali za kisheria," Anasema.

Tahadhari ya EWURA Kuhusu Biashara Haramu ya Mitungi ya Gesi

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Ziwa inaeleza kuwepo kwa baadhi ya wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu wanaojihusisha na biashara haramu ya mitungi ya gesi ya kupikia.

Akizungumza na waandishi wa habari mkoani Mara katika ukumbi wa Mwembeni Complex wakati wa mafunzo ya siku moja kuhusu majukumu, mafanikio, changamoto na mikakati ya EWURA katika sekta za nishati na maji, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, Nyirabu Musira, amesema mamlaka hiyo imebaini baadhi ya wafanyabiashara wakihamisha gesi kutoka mitungi mikubwa kwenda mitungi midogo kinyume cha sheria.

Amesema vitendo hivyo husababisha baadhi ya mitungi kuwa na ujazo usio sahihi na hivyo kuchangia malalamiko kutoka kwa wananchi.

Picha ya Nyirabu Musira, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa akitoa Mada kwa waandishi wa habari mkoa wa Mara katika mafunzo ya siku moja yaliyofanyika katika ukumbi wa Mwembeni Complex Manispaa ya Musoma

"Tunafahamu kuwa kuna watu wanafanya biashara haramu ya mitungi ya gesi kwa kuhamisha gesi kutoka mitungi mikubwa kwenda mitungi midogo kinyume na sheria na miongozo iliyopo. Tunawaomba wananchi kutoa taarifa EWURA wanapoona vitendo hivyo ili mamlaka ichukue hatua za kisheria," Amesema Musira.

Amefafanua kuwa mbali na kuathiri ujazo halisi wa gesi, vitendo hivyo vinahatarisha maisha ya wananchi kutokana na uwezekano wa milipuko na ajali za moto.

Musira amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwaeleza watoa huduma hiyo katika maduka, kupimiwa mitungi yao kwenye mizani kabla ya kuikabidhiwa ili kuhakikisha uzito unaendana na kiasi kilichoandikwa kwenye mtungi.

Nishati Safi ya Kupikia Yakua Tanzania

Tahadhari hii ya EWURA inakuja wakati Serikali ikiendelea kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

Kwa mujibu wa Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024–2034), idadi ya Watanzania wanaotumia nishati safi ya kupikia imeongezeka kutoka asilimia 1.5 mwaka 2010 hadi asilimia 6.9 mwaka 2021, ingawa kiwango hicho bado kiko chini sana ya wastani wa dunia wa asilimia 71.

Mkakati huo unaeleza kuwa takribani asilimia 90 ya kaya nchini bado zinategemea kuni na mkaa kama nishati kuu ya kupikia, huku asilimia 5.1 pekee zikitumia gesi ya LPG na asilimia 3 zikitumia umeme.

Serikali imeweka lengo la kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ifikapo mwaka 2034.

Matumizi ya Gesi LPG Yaongezeka

Takwimu za Wizara ya Nishati zinaonyesha matumizi ya gesi ya LPG nchini yameongezeka kwa kasi kutoka tani 20,000 mwaka 2010 hadi tani 160,610 mwaka 2022.

Hata hivyo pamoja na ongezeko hilo changamoto za gharama na upatikanaji bado zinaendelea kuwakabili watumiaji wengi. Mkakati wa Taifa unaonyesha gharama za kujaza mtungi mdogo ni kati ya shilingi 27,000 hadi 28,000 huku bei pia ikitegemea eneo na kampuni husika.

Kutokana na gharama hizo  watumiaji wengi wanatarajia kupata ujazo kamili wa gesi wanayolipia. Hivyo uwepo wa wafanyabiashara wanaodaiwa kuuza gesi yenye ujazo pungufu unaweza kuhujumu juhudi za Serikali za kuwahamasisha wananchi kuhamia kwenye nishati safi ya kupikia.

Bei za Gesi na Soko la Ushindani

Kuhusu  kupanda kwa bei za gesi, Meneja wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Kanda ya Ziwa Nyirabu Musira amesema, EWURA haipangi bei ya gesi ya LPG moja kwa moja kwa sababu bidhaa hiyo huagizwa kutoka nje ya nchi na kuuzwa katika mfumo wa soko huria la ushindani.

Amesema uwepo wa kampuni nyingi zinazotoa huduma ya gesi unampa mwananchi nafasi ya kuchagua kampuni yenye huduma bora na bei inayomfaa.

Hata hivyo amesema mamlaka itaendelea kusimamia usalama, ubora na uhalali wa biashara ya gesi ili kuhakikisha haki za watumiaji zinalindwa.

Kwa wananchi kama Jane na Monica, hatua hiyo inaweza kuwa mwanzo wa kurejesha imani yao katika matumizi ya gesi ya kupikia. Lakini kwa sasa, wanataka jambo moja tu; kila mtungi wa gesi unaonunuliwa uwe na ujazo kamili unaolingana na fedha walizolipa.












 

 

Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top