Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo, Mha. Athumani Kilundumya, amesema ushirikishwaji wa vijana katika kilimo biashara hatua muhimu ya kuchochea ukuaji wa uchumi wa Taifa pamoja na kuongeza ajira kwa vijana nchini.
Mha. Kilundumya amesema hayo tarehe 28 Mei 2026 jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kupata maoni ya vijana ambao wanafanya kilimo biashara katika mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo,mifugo na uvuvi; yakiwemo mashirika yasiyo ya kiserikali kuhusu mpango wa dhamana na mikopo ya kilimo biashara unaoandaliwa kupitia Mradi wa BBT Project I.
Amesema kuwa kikao hicho kina umuhimu mkubwa kwa maendeleo ya vijana na Taifa kwa ujumla kutokana na ukweli kuwa asilimia 34 ya Watanzania ni vijana. Ameeleza kuwa kundi hilo likiwezeshwa kushiriki katika shughuli za kilimo biashara litaweza kujitegemea kiuchumi, kuongeza Pato la Taifa.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imedhamiria kuwawezesha vijana nchini kupitia Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), na kuwajengea uwezo wa kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara. Hivyo, amehamasisha vijana pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali kuwasilisha maoni yao yatakayosaidia kuboresha mpango wa dhamana ya mikopo ya Kilimo.
Programu ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT) inalenga kuwasaidia vijana kushiriki katika biashara ndani ya mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi ili kuongeza ajira, kipato na maendeleo ya uchumi nchini.
✍️wizara ya kilimo


