Na Clement Robert, WAF - Dodoma
Serikali imedhamiria kuhakikisha kaya zote zisizo na uwezo nchini zinaingizwa katika mfumo wa Bima ya Afya kwa Wote ifikapo mwaka wa fedha 2028/29, hatua inayolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wenye hali duni ya kiuchumi.
Hayo yamebainishwa leo Mei 28, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa maelekezo ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti kuhusu Mpango wa Bima ya Afya kwa Wote.
Amesema, takwimu za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha asilimia 26.4 ya kaya Tanzania Bara sawa na kaya 3,917,457 ni kaya zisizo na uwezo, huku kati ya hizo, kaya 931,693 tayari zimetambuliwa na kukidhi vigezo vya kugharamiwa bima ya afya
“Serikali imepanga kutekeleza zoezi la utambuzi wa kaya zilizobaki kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka wa fedha 2026/27 hadi 2028/29 ili kuhakikisha wananchi wote wasiokuwa na uwezo wanapatiwa bima ya afya” amesema Mhe. Mchengerwa
Mhe. Mchengerwa amesema mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango huo Serikali itagharamia kaya 931,693 sawa na asilimia 24 ya kaya zote zisizo na uwezo nchini, ambapo kaya 276,004 tayari zimeanza kujumuishwa katika mfumo huo.
Amesema, uwekezaji mkubwa unaofanywa na Serikali katika sekta ya afya unaendelea kuwawezesha wananchi kupata huduma kuanzia ngazi ya zahanati hadi hospitali za rufaa za Taifa, huku takwimu za mahudhurio zikionesha wastani wa wagonjwa milioni 46 hutibiwa na kuruhusiwa kila mwaka na wagonjwa milioni 1.8 wakilazwa katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali imeendelea kutoa huduma za afya bila malipo kwa wananchi waliopo katika makundi maalum pamoja na wananchi wasiokuwa na uwezo wanaothibitishwa na Maafisa Ustawi wa Jamii.
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2025 zilizotolewa na Waziri huyo, jumla ya wagonjwa 269,322 walipatiwa matibabu katika hospitali za rufaa za Mikoa, Kanda, maalum na Taifa kwa utaratibu wa msamaha wa matibabu, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za afya bila kujali uwezo wao wa kifedha.
✍️wizara ya afya





