Rhobi Samwelly Awahimiza Viongozi wa UWT Kutoa Elimu ya Ukatili Katika Maeneo Yao

0


Na Mwandishi wetu, Mara. 

SHIRIKA  lisilo la Kiserikali linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia, la Hope for Girls and Women in Tanzania, limetoa wito kwa viongozi wa ngazi ya kata, wilaya na Mkoa wa Mara wa Jumuiya ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu kuhusu ukatili wa kijinsia. 

 Hatua hiyo itasaidia kuondoa vitendo hivyo vinavyoendelea kuathiri jamii na kurudisha nyuma juhudi za maendeleo zinazofanywa na serikali.

Wito huo umetolewa Juni 17, 2026 na Mkurugenzi wa Shirika hilo, Rhobi Samwelly, wakati akiwasilisha mada kuhusu “Wajibu wa Wanawake Viongozi kuhusu Ukatili wa Kijinsia” kwa viongozi wa UWT Mkoa wa Mara katika mafunzo yanayofanyika katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Songe iliyopo Manispaa ya Musoma.

Rhobi amesema, wanawake viongozi wana nafasi ya muhimu  katika jamii kutokana na ukaribu wao na wananchi, hivyo wanapaswa kutumia nafasi hiyo kutoa elimu kwa makundi mbalimbali kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia na namna ya kuuzuia.

Ameeleza kuwa, viongozi hao wana jukumu kubwa la kuwahamasisha wananchi na wanachama wa UWT katika maeneo yao kutambua haki za wanawake na watoto pamoja na kupinga mila na desturi kandamizi ambazo zimekuwa zikichangia kuendelea kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Amesema,  mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia yanahitaji ushirikiano wa wadau wote wakiwemo viongozi wa kisiasa, dini, mila na wananchi kwa ujumla ili kuhakikisha jamii inakuwa salama na yenye usawa.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa taarifa kwa wakati pindi matukio ya ukatili yanapotokea, akibainisha kuwa hatua hiyo itasaidia wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria na kuwapatia waathirika msaada unaostahili kwa wakati muafaka.

Kwa upande wao, baadhi ya viongozi wa UWT  wamepongeza juhudi za Hope for Girls and Women in Tanzania kwa kuendelea kutoa elimu inayolenga kulinda haki za wanawake na watoto, wakisema mafunzo hayo yatawaongezea uwezo wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi katika jamii.






Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top