Ghati Msamba, Mwanza.
Taasisi ya Angeline Foundation ya mkoa wa Mwanza inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya jamii, ikiwemo kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi kupitia ukarabati wa madawati, meza na viti katika shule mbalimbali za mkoa huo.
Akizungumza kwa njia ya simu na Musoma News Hub, Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Dk. Angeline Mabula,ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi,nyumba na Maendeleo ya makazi alisema lengo la kuanzishwa kwa taasisi hiyo ni kushughulikia masuala mbalimbali ya maendeleo ya jamii, hususan elimu, afya na utoaji wa misaada ya ada kwa watoto wanaotoka katika mazingira magumu.
Dk. Mabula alisema kwa sasa taasisi hiyo imefadhili kikundi cha vijana cha Agro Tech kutoka mkoani Mtwara, ambacho kinajishughulisha na ukarabati wa madawati yanayoharibika mashuleni.
"Baada ya kukiona kikundi hiki kupitia mitandao ya kijamii na kufuatilia kazi wanazozifanya kwa kujitolea, tuliwasiliana nao na walikubali kuja Mwanza kusaidia ukarabati wa madawati, meza na viti katika shule mbalimbali," alisema Dk. Mabula.
Kwa upande wake, Katibu Mtendaji Mkuu wa Angeline Foundation, Charles David, alisema mkurugenzi wa taasisi hiyo alivutiwa na uzalendo na moyo wa kujitolea uliooneshwa na vijana wa Agro Tech, jambo lililomfanya kuwasiliana nao pamoja na viongozi wa serikali za mitaa ili kuwezesha utekelezaji wa mradi huo.
"Baada ya kuona kazi nzuri wanayoifanya vijana hawa, mkurugenzi alifanya mawasiliano na wakurugenzi wa halmashauri pamoja na viongozi wa wilaya. Vijana hao walikubali kwa moyo wa dhati kuja Mwanza kusaidia kuboresha madawati, meza na viti katika shule za Halmashauri ya Jiji la Nyamagana," alisema David.
Aidha, alitoa wito kwa wadau mbalimbali wa maendeleo kujitokeza na kuunga mkono juhudi za vijana hao kwa kuwa kazi wanayoifanya ni ya kizalendo na ina mchango mkubwa katika kuboresha mazingira ya elimu.
Alisema Angeline Foundation ilianza shughuli zake mwaka 2012 na ina uwezo wa kupanua huduma zake katika mikoa mingine nchini endapo itapata wadhamini wa kutosha.
Naye mwakilishi wa kikundi cha Agro Tech kutoka mkoani Mtwara, Juma Kassim, alimshukuru Dk. Angeline Mabula kwa kuwadhamini kufika Mwanza na kuendelea na shughuli za ukarabati wa madawati, meza na viti katika shule mbalimbali.
Kassim aliwahimiza vijana wengine kujitokeza na kushiriki katika shughuli za kujitolea zinazolenga kuleta maendeleo ya jamii, akibainisha kuwa ukarabati wa madawati hupunguza gharama kubwa za kutengeneza madawati mapya.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Fumagila, Dotto Gibebe, alisema shule hiyo imepokea mradi huo kwa furaha kubwa kutokana na changamoto ya madawati zaidi ya 200 yaliyokuwa yameharibika.
"Mradi huu umetupa faraja kubwa kwa kuwa unasaidia kurejesha madawati yaliyokuwa yameharibika na kupunguza gharama za kununua au kutengeneza mapya," alisema Gibebe.
Aliishukuru Angeline Foundation kwa kuleta kikundi hicho shuleni hapo na kuwataka walimu wakuu wa shule nyingine ambazo bado hazijafikiwa na mradi huo kuandaa vifaa vya msingi vya ukarabati, ikiwemo mbao, misumari na vifaa vya kuchomelea, ili kurahisisha utekelezaji wa kazi hizo na kupunguza gharama za matengenezo.
Mradi huo unatarajiwa kuwanufaisha mamia ya wanafunzi kwa kuboresha mazingira ya kujifunzia na kuongeza ufanisi wa elimu katika shule mbalimbali za mkoa wa Mwanza.







