Na Atley Kuni, Shanghai, China
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Dawa na Vifaa Tiba, Bw. Emmanuel Tayari, amesema Tanzania imejipanga kuwa kitovu kikuu cha uzalishaji wa dawa barani Afrika kutokana na ongezeko kubwa la mahitaji ya bidhaa za afya na mageuzi ya kimkakati katika sekta ya dawa.
Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Dawa ya CPHI China 2026 yanayoendelea jijini Shanghai, Bw. Tayari ameisema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia wazalishaji wa kimataifa kuwekeza katika viwanda vya dawa, malighafi na bidhaa za afya nchini.
Amebainisha kuwa mahitaji ya dawa nchini yanatarajiwa kuongezeka kutoka takribani pakiti milioni 131 mwaka 2024/25 hadi zaidi ya pakiti milioni 600 ifikapo 2039/40, hali inayoonyesha ukuaji mkubwa wa soko na fursa za uwekezaji wa muda mrefu.
Bw. Tayari amesema Bohari ya Dawa (MSD) hununua bidhaa za afya zenye thamani ya takribani dola za Marekani milioni 491 kwa mwaka, jambo linalotoa uhakika wa soko kwa wazalishaji wa ndani na wa kimataifa wanaotaka kuwekeza nchini.
Aidha, amefafanua kuwa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) imefikia Kiwango cha Tatu cha Ukomavu cha Shirika la Afya Duniani (WHO Maturity Level 3), hatua inayoongeza imani ya wawekezaji kuhusu ubora na usalama wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
"Serikali imepunguza muda wa usajili wa bidhaa za dawa zinazozalishwa nchini hadi siku 60, sambamba na kuanzisha maeneo maalum ya viwanda vya dawa Mloganzila na Kibaha ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya uwekezaji", amesema Tayari.
Bw. Tayari amesisitiza kuwa Tanzania ina nafasi ya kipekee kama lango la biashara ya dawa katika masoko ya kikanda kupitia Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC, vinavyounganisha soko la zaidi ya watu milioni 780.
Amehitimisha kwa kusisitiza kuwa Serikali itaendelea kulinda wazalishaji wa ndani na kuhakikisha mazingira ya ushindani wa haki, huku akiwataka wawekezaji kutumia fursa zilizopo nchini kwa manufaa ya muda mrefu ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
✍️wizara ya afya





