Na Emmanuel Chibasa
Hedhi
ni sehemu ya kawaida ya maisha ya mwanamke na msichana, lakini kwa maelfu ya
watoto wa kike nchini Tanzania bado ni chanzo cha changamoto kinachoathiri
afya, elimu, utu na ustawi wao.
Kwa
baadhi ya wasichana, hedhi ni mchakato wa kibaiolojia wa kawaida, lakini kwa
wengine imekuwa kikwazo kinachowafanya kukosa masomo, kupoteza kujiamini na
kushindwa kushiriki kikamilifu katika maisha ya shule.
Kwa
mujibu wa Wizara ya Afya Tanzania, takribani wasichana na wanawake milioni 15
kati ya watu milioni 61.7 hupitia hedhi na Ili kusimamia hedhi kwa usalama na
utu, wasichana na wanawake wanahitaji upatikanaji wa taarifa sahihi, huduma za
maji safi na usafi, mazingira rafiki pamoja na vifaa salama vya kujisitiri.
Katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, haki za hedhi salama
zinaweza kutafsiriwa ndani ya haki za afya ya umma na haki za binadamu. Ibara
ya 9(a) na (f) inaeleza kuwa mamlaka za dola na taasisi zake zinapaswa
kuelekeza sera na mipango yake katika kuhakikisha utu wa binadamu na haki
nyingine za msingi zinaheshimiwa na kulindwa, ikiwemo haki ya afya na elimu kwa
wote.
Pamoja
na jitihada zinazofanywa na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali wa maendeleo kuboresha afya na usafi wa hedhi, changamoto bado
zinaendelea kujitokeza hasa kwa watoto wa kike wanaotoka katika familia zenye
kipato cha chini. Ambapo hali hii husababisha baadhi ya wanafunzi kushindwa
kuhudhuria masomo wakati wa hedhi kutokana na ukosefu wa taulo za kike.
Katika Shule ya Msingi Kwangwa “A” iliyopo Kata ya Kwangwa Manispaa ya Musoma mkoani Mara, changamoto hiyo imeendelea kuwa kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanafunzi wa kike katika safari yao ya elimu katika shule hiyo yenye jumla ya wanafunzi 1, 507, Wasichana wakiwa 738 na wavulana 769 kama wanavyoeleza Lightness Jumapili,Gladness Jackson, Maria Peter pamoja na Gloria Amos.
Lightness
Jumapili, mwenye umri wa miaka 14, mkazi wa Mshikamano na mwanafunzi wa darasa
la saba katika Shule ya Msingi Kwangwa “A”, anasema moja ya changamoto kubwa
wanazokutana nazo wasichana shuleni hapo ni kukosa masomo wanapoingia katika
siku zao za hedhi kutokana na kukosa taulo za kike na fedha za kununua vifaa
hivyo.
Anasema wakati mwingine msichana anaweza kuingia katika siku zake akiwa shuleni bila kutarajia na kujikuta amechafuka nguo bila kuwa na nguo za kubadilisha. Hali hiyo huwasababishia aibu kubwa mbele ya wanafunzi wenzao na wakati mwingine hulazimika kuondoka shuleni kabla ya muda.
Kwa
mujibu wa Lightness, changamoto hiyo imekuwa ikiathiri ushiriki wao darasani na
kuwafanya baadhi ya wasichana kupoteza kujiamini kabisa mbele ya wenzao.
“Naiomba
serikali na mashirika mbalimbali kutusaidia sisi wasichana kwa sababu sisi ndio
viongozi wa baadaye. Tunahitaji kupata taulo za kike ili tuweze kuhudhuria
masomo kama wanafunzi wengine,” Anasema Lightness.
Kwa
upande wake Gladness Jackson mwenye umri wa miaka 12, anayesoma darasa la tano
katika Shule ya Msingi Kwangwa “A”, anasema wasichana wengi wanapitia
changamoto mbalimbali wanapoingia katika hedhi.
Anasema
wakati mwingine mwanafunzi anaweza kuingia katika siku zake lakini akaogopa
kuingia darasani au kukaa karibu na wanafunzi wengine kwa hofu ya kuchafuka na
kuchekwa na wenzake na changamoto huwa kubwa zaidi pale ambapo mzazi au mlezi
hana uwezo wa kununua taulo za kike.
“Msichana
anaweza kumweleza mzazi kuwa ameingia katika siku zake lakini akaambiwa hakuna
fedha za kununua taulo za kike. Tunaomba wazazi waelimishweshe kuhusu hedhi
salama na kuhakikisha wanatusaidia kupata vifaa salama vya kujisitiri,” Anasema
Gladness.
Maria
Peter, mwenye umri wa miaka 12 na mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya
Msingi Kwangwa “A”, anasema changamoto ya kukosa taulo za kike imekuwa
ikiwafanya baadhi ya wanafunzi hukaa nyumbani
kwa siku kadhaa kila mwezi kwa sababu ya kukosa vifaa vya kujisitiri, hali
inayowafanya kubaki nyuma katika masomo ikilinganishwa na wenzao.
“Tunaomba
serikali na mashirika binafsi waendelee kutusaidia kupata taulo za kike ili
tuweze kujisitiri wakati wa hedhi na kuendelea na masomo yetu kwa sababu sisi
ndio taifa la kesho,” Anasema Maria.
Naye
Gloria Amos mwenye umri wa miaka 12, anayesoma darasa la sita katika shule
hiyo, anasema changamoto za hedhi haziishii tu kwenye kukosa taulo za kike bali
pia huathiri usalama na mustakabali wa wasichana.
Anasema
baadhi ya wasichana hukumbana na vishawishi kutoka kwa vijana wa kiume
wanapokosa mahitaji ya msingi hali inayoweza kuwaweka katika hatari ya mimba za
utotoni na hatimaye kukatiza masomo yao.
“Wasichana
wengi wanahitaji msaada wa taulo za kike ili waendelee na masomo. Tunaomba
serikali na mashirika mbalimbali waendelee kutusaidia kwa sababu changamoto
bado ni kubwa,” Anasema Gloria.
Kauli
za wasichana hao toka shule ya msingi Kwangwa “A” zinaonyesha wazi namna hedhi
inavyoweza kuwa kikwazo kikubwa kwa elimu ya mtoto wa kike pale ambapo
mazingira salama na vifaa vya kujisitiri vinapokosekana.
Kulwa
Gervas ni mwalimu ambaye pia ni mwalimu wa ushauri nasaha katika Shule ya
Msingi Kwangwa “A”, anasema changamoto ya wanafunzi wa kike kushindwa
kuhudhuria masomo wakati wa hedhi bado ni kubwa kutokana na hali za kiuchumi za
baadhi ya familia na mara nyingi wanafunzi hukosa kueleza sababu halisi za
kutokuwepo shuleni kwa hofu au aibu.
“Wakati
mwingine mwanafunzi anarudi shule baada ya siku kadhaa na ukimuuliza anakueleza
kuwa alikuwa kwenye siku zake lakini hakupata taulo za kike. Wengine huambiwa
kutumia vitambaa vya kawaida ambavyo muda mwingine sio salama.
Tunaiomba
serikali na wadau kuongeza uwekezaji katika shule za msingi sababu tunaona
nguvu kubwa inaelekezwa katika shule za Sekondari, huku katika shule za msingi changamoto
ni kubwa kuliko inavyofikiriwa,” Anasema Kulwa.
Kulwa
anaongeza kuwa watoto wanaanza kubalehe katika umri mdogo zaidi kuliko
zamani hali inayokdiriliwa kuwa zaidi
aslimia hamsini ya wasichana hukosa masomo katika shule hiyo kutokana na changamoto ya
hedhi jambo linaloongeza uhitaji wa msaada wa taulo za kike na elimu ya hedhi
salama zaidi katika shule za msingi.
Rose
Nyamhanga ni mama wa watoto watatu mkazi wa Mwisenge manispaa ya Musoma mzazi
wa mmoja wa wanafunzi wa Shule ya anasema changamoto ya kipato imekuwa
ikiwafanya baadhi ya wazazi kushindwa kumudu gharama za kununua taulo za kike
kila mwezi.
“Tunawashukuru
wadau wanaotusaidia kwa sababu kuna wazazi ambao hawawezi kumudu gharama hizi
kila mwezi. Msaada huu unawasaidia watoto wetu kuendelea na masomo,”
Changamoto
ya hedhi salama inayowakabili wasichana wa Kwangwa inaakisi hali inayoshuhudiwa
sehemu mbalimbali nchini.
Akizungumza
katika maadhimisho ya Siku ya Hedhi Salama Duniani yaliyofanyika wilayani
Kibondo mkoani Kigoma, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya
Waziri wa Afya Mhe. Mohamed Mchengerwa, alitoa wito kwa jamii, taasisi za umma
na binafsi kushirikiana kuondoa unyanyapaa wa hedhi na kuhakikisha huduma
rafiki za hedhi salama zinapatikana kwa wanawake na wasichana ili kuwawezesha
kuishi kwa utu, usalama na heshima.
Dkt.
Samizi alisema hedhi ni mabadiliko ya kawaida ya kibayolojia na si ugonjwa wala
jambo la kuaibisha, hivyo jamii inapaswa kuondoa mila potofu na unyanyapaa
unaowakwamisha wasichana kushiriki kikamilifu katika shughuli za kijamii na
kielimu.
Alieleza
kuwa tafiti zinaonesha asilimia 27 ya wasichana nchini hukosa shule angalau
siku tatu kila mwezi kutokana na changamoto za hedhi, jambo linalowapotezea
zaidi ya siku 30 za masomo kwa mwaka na kuathiri maendeleo yao kitaaluma.
Kwa
mujibu wa Dkt. Samizi, Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha
miundombinu rafiki ya hedhi salama ikiwemo ujenzi wa vyoo bora vyenye huduma ya
maji, usafi na mazingira salama ya kujifunzia mashuleni ili kulinda afya, utu
na heshima ya wanawake na watoto wa kike nchini.
Bakari
Nyamsosa ni Mkurugenzi wa shirika la Rising Hope Organization Tanzania lenye
makao yake makuu Manispaa ya Musoma Mkoani Mara, Akizungumza na Musoma Tv mara
baada ya kutoa msaada na kugawa taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya msingi
Kwangwa “A” anasema shirika hilo lilianza programu ya kugawa taulo za kike
baada ya kubaini idadi kubwa ya wasichana kukosa masomo katikati na mwishoni
mwa mwezi.
Anasema utafiti wao ulibaini kuwa sababu kubwa ilikuwa ni ukosefu wa taulo za kike, jambo lililosababisha wasichana kukosa shule kwa siku nne hadi tano kila mwezi.
Kutokana na hali hiyo, Rising Hope Organization ilianza kugawa taulo za kike mashuleni ili kuongeza mahudhurio na kuimarisha kujiamini kwa wasichana.
“Baada ya kuanza kutoa taulo za kike tumeshuhudia ongezeko la mahudhurio ya wasichana shuleni. Lakini mahitaji bado ni makubwa kuliko uwezo wetu. Tunahitaji ushirikiano wa serikali na wadau ili kuwafikia wasichana wengi zaidi,” Amesema Bakari.
Kwa
mujibu wa Wizara ya Afya Tanzania hedhi isiyo salama inaweza kusababisha
maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), magonjwa ya mfumo wa uzazi na kuathiri maendeleo
ya mwanamke kielimu, kijamii na kiuchumi.
Wizara ya Afya inahimiza jamii kuwasaidia wasichana kumudu hedhi kwa njia salama na yenye utu, huku wazazi, walimu na jamii wakihimizwa kutoa elimu sahihi kuhusu hedhi na balehe.
Kila
mwaka Mei 28 huadhimishwa Siku ya Hedhi Salama Duniani kwa lengo la kuongeza
uelewa, kupinga unyanyapaa na kuhamasisha upatikanaji wa huduma rafiki za hedhi
kwa wasichana na wanawake.
Kaulimbiu ya mwaka 2026 ni: “Wezesha Mazingira ya Hedhi Salama yenye Utu kwa Wasichana na Wanawake Wote.”
Kwa
wasichana wa Kwangwa, kaulimbiu hiyo si maneno tu bali ni matumaini ya siku
zijazo ambapo hakuna mtoto wa kike atakayelazimika kukosa masomo, kupoteza
kujiamini au kuacha ndoto zake kwa sababu ya kukosa taulo za kike.













