Na Ghati Msamba
MATUMIZI sahihi ya mifumo ya kidijitali, kuzingatia taratibu za utumishi wa umma na kuimarisha mawasiliano kati ya taasisi za serikali na Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora vimetajwa kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi
Maelekezo hayo yalitolewa Juni 1, 2025 jijini Dodoma wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Mwaka wa Maafisa Tawala na Rasilimali Watu uliofanyika katika Ukumbi wa Gen. Mabeyo na kuwakutanisha wataalamu kutoka wizara, idara, taasisi za serikali zinazojitegemea pamoja na mamlaka za serikali za mitaa.
Akizungumza katika mkutano huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, aliwataka maafisa hao kuendelea kufuata taratibu za utumishi wa umma na kuimarisha ushirikiano na mawasiliano kati ya ofisi zao na Ofisi ya Rais – Utumishi ili kurahisisha utatuzi wa changamoto zinazojitokeza katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisisitiza umuhimu wa matumizi ya teknolojia za mawasiliano na mifumo mbalimbali iliyoandaliwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, akieleza kuwa mifumo hiyo imewekwa kwa lengo la kuongeza ufanisi, uwajibikaji na kurahisisha utoaji wa huduma ndani ya utumishi wa umma.
Mkutano huo wa mwaka, unaoandaliwa na Ofisi ya Rais – Utumishi na Utawala Bora, umekuwa jukwaa muhimu la wataalamu wa utawala na rasilimali watu kujadili changamoto zinazowakabili katika utekelezaji wa majukumu yao pamoja na kubadilishana uzoefu wa namna bora ya kuzikabili.
Katika hotuba yake, Waziri huyo pia alieleza mafanikio yaliyofikiwa na serikali katika kuboresha utumishi wa umma, yakiwemo ujenzi na uimarishaji wa mifumo ya kiutendaji, upandishaji wa madaraja kwa watumishi pamoja na ulipaji wa madeni yanayotokana na mishahara na likizo.
Aidha, alitumia fursa hiyo kutoa shukrani kwa Samia Suluhu Hassan kwa maelekezo na usimamizi wake ambao umechangia kuimarika kwa utendaji kazi serikalini na kuboresha huduma zinazotolewa kwa wananchi.
Mkutano huo unatarajiwa kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha zaidi usimamizi wa rasilimali watu na kuongeza tija katika utumishi wa umma nchini.







