Wanawake wengi nchini Tanzania wamekuwa wakijishughulisha
na biashara ndogo ndogo ili kujipatia kipato cha kujikimu na kuendesha familia
zao. Miongoni mwa biashara hizo ni uuzaji wa mboga mboga na matunda katika
masoko na mitaa mbalimbali wanayoishi. Biashara hii imekuwa chanzo muhimu cha
kipato kwa wanawake wengi, licha ya kukabiliwa na changamoto mbalimbali za
kiuchumi na kijamii.
Katika kufanya makala hii, nilifanya mahojiano na
mwanamke muuza mboga mboga mkazi wa Tandale jijini Dar es Salaam, anayeitwa
Ester George, mama wa watoto watatu. Ester anaendesha biashara yake ndogo ya
kuuza mboga na matunda ili kusaidia mahitaji ya familia yake. Anasema kuwa
alianza biashara hiyo miaka kadhaa iliyopita baada ya kuona kipato cha familia
hakitoshi kukidhi mahitaji ya kila siku.
Katika mahojiano hayo, Ester anaeleza kuwa biashara ya
mboga mboga na matunda imekuwa msaada mkubwa katika familia yake. “Kupitia
biashara hii naweza kununua chakula nyumbani, kusaidia ada za watoto na gharama
nyingine za familia. Mume wangu hana kazi yenye kipato kikubwa, hivyo biashara
yangu imekuwa msaada mkubwa kwa familia yetu,” anasema Ester.
Licha ya mchango huo, wanawake wengi wanaofanya biashara
ya mboga na matunda hukumbana na changamoto mbalimbali. Miongoni mwa changamoto
hizo ni mtaji mdogo, ushindani mkubwa katika masoko, pamoja na uharibifu wa
bidhaa hasa matunda na mboga zinazoharibika haraka. Pia wateja wengine huchukua
bidhaa kwa mkopo lakini hushindwa kulipa kwa wakati, jambo linalopunguza mtaji
wa wafanyabiashara hawa.
Mbali na changamoto hizo za kiuchumi, wanawake hawa pia
hukumbana na changamoto za unyanyasaji wa kijinsia katika maeneo yao ya kazi.
Baadhi yao hukumbana na maneno ya kudhalilisha, vitisho au hata vishawishi
visivyofaa kutoka kwa baadhi ya wanaume wanaowazunguka katika maeneo ya
biashara. Ester anaeleza kuwa hali hiyo wakati mwingine huwafanya wanawake
kufanya kazi katika mazingira yasiyo salama. Kwani yeye amekuwa ni mmoja kati
ya wahanga waliokumbana na changamoto hizo ikiwemo kuitwa majina yasiyofaa na
wakati mwingine baadhi ya watu kumdhania kwamba yeye si mwanamke anayependa
kutulia nyumbani kwake.
Kwa upande wa serikali, juhudi mbalimbali zimekuwa
zikifanyika kusaidia wanawake wafanyabiashara wadogo. Afisa wa maendeleo ya
jamii na ustawi wa jamii katika halmashauri anasema wao hutoa elimu kuhusu haki
za wanawake, mbinu za kujilinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia, pamoja na
kuwahamasisha wanawake kujiunga katika vikundi vya kiuchumi ili waweze kupata
mikopo ya riba nafuu. Pia serikali imekuwa ikitoa mafunzo ya ujasiriamali ili
kuwasaidia wanawake hawa kuboresha biashara zao.
Wadau
wengine ambao wamekuwa wakitetea haki na usawa wa wanawake nchini ikiwemo Chama
cha Wanawake Wanahabari Tanzania (TAMWA), kupitiaMkurugenzimtendajiwataasisihiyo
Dr. Rose Reuben katika kilelehicho cha siku ya wanawake amesema licha ya uwepo wa
changamoto nyingi kwa wanawake wauzaji wa mbogamboga ikiwemo upungufu wa usalama
, kukosekana kwa soko la uhakika na hata upatikanaji hafifu wa bidhaa lakini bado
wanaendelea kuwapa elimu wakishirikiana na benki ya CRDB kwani wanawake wengi wajasiriamali
wameahidi kupokea elimu hiyo na kuendelea kuitumia huku kipaumbele cha
mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kikizingatiwa ili kufikia usawa katika
Nyanja zote za kijamii.
Aidha,
taasisi mbalimbali za kifedha ikiwemo
Benki ya CRDB imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake
wajasiriamali kupitia huduma za kifedha jumuishi, mikopo nafuu, pamoja na
mafunzo ya ujasiriamali ikiwemo kupitia programu zake mbalimbali. CRDB katika siku maalumu
ya wanawake duniani ambayo waliungana na wanawake wajasiriamali kwa kushirikianana
TAMWA kupitia Meneja usimamizi wa mafunzo ambaye ni Joshua Mwakalobo amesema wataendelea
kutoa elimu ya fedha na ujasiriamali ili kuwainua vijanana wanake wajasiriamal ipamoja
na kuwawezesha kifedha ili kuijua thamani ya pesa n amafanikio.
Kwaujumla benki hiyo imefanikiwa kuwainua wanawake hawa
kwa kuwapatia mitaji na ujuzi unaowawezesha kukuza biashara zao, kuongeza
kipato, na kuboresha maisha yao na jamii inayowazunguka kwa ujumla.
Wanawake wanaouza mboga mboga na matunda pia wana mchango
mkubwa katika jamii na uchumi. Wanachangia upatikanaji wa chakula kwa urahisi
katika maeneo ya mijini na vijijini, wanazalisha ajira binafsi, na kusaidia
familia zao kupata mahitaji muhimu kama chakula, elimu na huduma za afya.
Biashara hizi ndogo ndogo pia huchangia mzunguko wa fedha katika jamii.
Katika mafanikio hayo, mchango wa wanaume nao ni muhimu.
Wanaume wanaweza kuwasaidia wake zao kwa kuwapa ushirikiano, kuwaheshimu katika
kazi zao, pamoja na kuwasaidia katika majukumu ya familia ili wanawake waweze
kuendesha biashara zao kwa utulivu. Ushirikiano wa wanandoa katika shughuli za
kiuchumi unaweza kuimarisha ustawi wa familia kwa ujumla.
Kutokana na hali hiyo, jamii inapaswa kuthamini na
kuheshimu kazi zinazofanywa na wanawake hawa, huku ikiendelea kupinga vitendo
vyote vya unyanyasaji wa kijinsia. Wanawake nao wanahimizwa kuendelea kufanya
kazi kwa bidii, kujiunga katika vikundi vya maendeleo na kutumia fursa za
mafunzo na mikopo zinazotolewa na serikali na taasisi mbalimbali. Kwani takwimu
mbalimbali za kiuchumi ikiwemo Global Enterpreneurship kwa mwaka 2024 inaonesha
kuna ongezeko la wanawake katika umiliki wa biashara ndogo ndogo ambazo zimekua
ni sehemu mojawapo inayochangia kukua kwa uchumi wa mtu mmoja mmoja, familia na
hata Taifa kwa ujumla.
Kwa ujumla, wanawake wauzaji wa mboga mboga na matunda ni
sehemu muhimu ya maendeleo ya familia na jamii. Kwa kupewa mazingira salama ya
kufanya biashara pamoja na msaada kutoka kwa jamii na serikali, wanaweza
kuendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa katika ukuaji wa uchumi wa nchi, wakati
nchi ikikua ni vyema kuhakikisha usalama wa wanawake na jamii nzima kwa ujumla.
Kwa pamoja TUMLINDE MWANAMKE ILI TUILINDE JAMII YETU SOTE.


