Na Angela Sebastian
Bukoba : Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Kagera,Nazir Karamagi, ameongoza Kamati ya Siasa ya Mkoa huo kutembelea na kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba ikiwa ni utaratibu wa chama hicho kufuatilia utekelezaji wa Ilani ya CCM ili kuhakikisha miradi inanufaisha wananchi.
Katika ziara hiyo, kamati ilitembelea mradi wa ghala la kuhifadhia dagaa uliopo katika Mwalo wa Rukojo, Kata ya Kaagya uliogharimi zaidi ya shilingi milioni 100 pia, ilikagua ujenzi wa shule ya msingi Kamagoba ambao umegharimu zaidi ya shl mil. 300 ambapo Karamagi amemshukuru Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi hicho cha pesa ili kufanikisha miradi hiyo yenye manufaa kwa jamii.
Pia ameupongeza uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba kwa usimamizi mzuri wa miradi ya maendeleo sambamba na kutenga fedha ya mapato ya ndani kutekeleza miradi mbalimbali kwa ufanisi wa hari ya kulidhisha huku, akisisitiza umuhimu wa kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi ili kuhakikisha fedha za Serikali zinazotokana na kodi za Watanzani zinaleta matokeo yaliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi.
Baadhi ya Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba hususani diwani wa Kata ya Kaagya ulipo mradi wa ghala la kuhifadhia dagaa Stanley Nestory walimpongeza Rais Dk. Samia kwa kuendelea kutenga fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo,hari inayochangia kuboresha huduma za kijamii na kuinua maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri hiyo.
Nestory amesema mradi huo unatarajiwa kuingizia Halmashauri hiyo mapato kati ya shil mil. 25 hadi 40 kwa mwezi ambapo asilimia 30 inabaki kwenye kijiji na 70 inachukuliwa na Halmashauri kwasababu wanaenda kufanya uhifadhi wa dagaa wa kisasa kutokana na dagaa kutonyeshewa na mvua hari iliyokuwa ikiwasababishia hasara kubwa.









