Waziri wa Kilimo, Mhe. Daniel Chongolo (Mb), amekutana kwa mazungumzo na ujumbe ulioongozwa na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Frontier, Bw. Lars Tushuizen tarehe 11 Juni 2026, jijini Dodoma ambao wana nia ya kuwekeza katika Sekta ya Kilimo.
Mazao hayo ni Parachichi na Chai ambapo wamejadili kuimarisha uzalishaji, kuongeza thamani na kupanua wigo wa masoko ya ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya wakulima na maendeleo ya Sekta ya Kilimo nchini.
Bw. Lars Tushuizen ameeleza kuwa Kampuni yake inalenga kuendeleza mnyororo wa thamani wa mazao hayo kupitia uwekezaji wa matumizi ya teknolojia za kisasa. Ameeleza kuwa amevutiwa kuwekeza nchini kwa kuwa Tanzania ina mazingira mazuri ya uwekezaji na fursa kubwa za uzalishaji wa Parachichi na Chai, ambapo fursa hizo zinaweza kuchangia kuongeza mapato ya wakulima na ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Mhe. Waziri Chongolo amekaribisha uwekezaji na kuahidi kuwa Serikali itatoa ushirikiano kwa wawekezaji hao na wengine wowote wenye dhamira ya kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini. Amesisitiza kuwa Wizara ya Kilimo itaendelea kuweka mazingira wezeshi yatakayovutia wawekezaji, kuimarisha ushindani wa mazao yanayozalishwa Tanzania katika masoko ya Kimataifa ili kuleta tija kwa wakulima na Taifa kwa ujumla.
Washiriki katika Mkutano huo ni Mha. Athumani Kilundumya, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Umwagiliaji na Zana za Kilimo; Prof. Peter L. M. Msoffe, Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Maendeleo ya Mazao na Usalama wa Chakula; Bi. Beatrice Banzi, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania; wakiwemo Maafisa Waandamizi wa Wizara ya Kilimo.
✍️wizara ya kilimo


