Wizara ya Kilimo inaendelea na zoezi la ukusanyaji wa sampuli kwa ajili ya upimaji wa afya ya udongo katika mikoa ya Njombe, Iringa, Mbeya, Songea, Katavi na Rukwa.
Zaidi ya sampuli 28,027 zinatarajiwa kukusanywa zikijumuisha sampuli 1,221 kutoka katika mashimo makubwa (soil profile) na sampuli 12,182 kutoka katika mashimo mafupi (observation points) kwa mikoa yote sita.
Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya Bw. Rodrick Mpogolo amezungumza tarehe 01 Juni 2026 mkoani humo wakati wa kikao elekezi cha utekelezaji huo na kueleza kuwa zoezi hilo ni muhimu katika kufikia Dira 2050 kwa kuwa kilimo kinapaswa kufanyika kisayansi.
Amesema upimaji wa afya ya udongo utaiwezesha Tanzania kufikia kipato cha kati ngazi ya juu, kutokomeza umaskini kwa makundi yote pamoja na kuiwezesha Tanzania kuwa mzalishaji mkuu wa chakula Barani Afrika na miongoni mwa nchi 10 bora Duniani.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi na Mipango ya Matumizi ya Ardhi ya Kilimo Mhandisi Juma Mdeke, amewakumbusha wataalamu wanaoshiriki katika zoezi hilo kuwa tayari kujifunza kwa kuzingatia weledi na uwajibikaji.
Ameeleza kuwa upimaji wa afya ya udongo nchini umeshafanyika katika mikoa 19 ya Tanzania Bara ikiwemo Kilimanjaro; Arusha; Kagera; Kigoma; Mara; Mwanza; Geita; Manyara; Simiyu; Shinyanga; Singida;Tabora; Dodoma; Morogoro; Tanga; Pwani; Lindi; Mtwara na Ruvuma.
✍️wizara ya kilimo


