Benki ya Kimataifa ya Japan inayoitwa Sumitomo Mitsui Banking Corporation (SMBC) imeonesha utayari wa kuwekeza katika Sekta ya Kilimo nchini kupitia uwezeshaji wa upatikanaji wa mitaji kwa ajili ya ununuzi wa matrekta yatakayochangia kuongeza tija na kuimarisha uzalishaji wa kilimo.
Akizungumza na ugeni kutoka nchini Japan tarehe 12 Juni 2026 jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli, amesema mpango uliyowasilishwa na Benki hiyo unaendana na malengo ya Serikali ya kuwa na uwekezaji wa matrekta 10,000 hadi ifikapo mwaka 2030 hatua itayowawezesha wakulima kupata huduma ya zana za kısasa za kilimo kupitia vituo vya zana za kilimo nchi nzima.
Ujumbe wa benki hiyo umeongozwa na Makamu Mkurugenzi wa SMBC, Bw. Taro Otsu, ambaye amesema SMBC ina dhamira ya kuwezesha upatikanaji wa mkopo utakaosaidia ununuzi wa matrekta hayo ili kukuza Sekta ya Kilimo nchini. Ameeleza kuwa benki hiyo iko tayari kushirikiana na Serikali katika kubaini utaratibu unaofaa wa utekelezaji wa mpango huo.
Aidha, ameeleza kuwa kuna njia mbalimbali zinazoweza kutumika katika utoaji wa mkopo huo, ikiwemo kupitia taasisi za kifedha za ndani au kwa utaratibu utakaoafikiwa kwa kushirikiana na Serikali.
Katibu Mkuu Mweli ambaye amemwakilisha Mhe. Daniel Chongolo, Waziri wa Kilimo katika mazungumzo hayo, ameishukuru benki hiyo kwa kuonesha nia ya kuwekeza na kueleza kuwa wadau muhimu wakiwemo Wizara ya Fedha na Tume ya Taifa ya Mipango watashirikishwa ili kubaini namna bora ya ushirikiano kwa kuzingatia maslahi mapana na wakulima na Taifa kwa ujumla.
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na wawakilishi kutoka Kampuni ya Kubota; Kampuni ya Agricom; Mfuko wa Udhamini wa Pembejeo za Kilimo (AGITF); Benki ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania; na Wakurugenzi wa Wizara ya Kilimo.
✍️wizara ya kilimo


