Na Angela Sebastian
Bukoba: Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoani Kagera imefanikisha kurejesha zaidi ya shilingi milioni 624.6 baada ya kushinda kesi 50 kati ya 52 zilizoendeshwa katika mahakama mbalimbali za mkoa wa kagera kwa kipindi cha Julai 2025 hadi sasa.
Akitoa taarifa ya kipindi cha kuanzi Januari hadi Machi mwaka huu kwa waandishi wa habari wa vyombo mbalimbali vya habari mjini Bukoba,Naibu mkuu wa Takukuru mkoani humo Leonard Swai ameeleza kuwa,kwa kipindi cha Julai 2025 hadi sasa walifanikiwa kufungua kesi 61 mahakamani ambapo mashauri 52 yameamuliwa kati ya hayo takukuru imeshinda mashauri 50 sawa na asilimia 97 ,imeshindwa mashauri mawili na mashauri 9 yanaendelea mahakamani.
Amesema katika mashauri 50 ambayo Takukuru imeshinda wamefanikiwa kurejesha kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 624.6 ambapo kwa Januari hadi Machi 2026 wamepokea taarifa 132 kati ya hizo 83 zilihusu rushwa na taarifa 49 hazikuhusu rushwa.
Alieleza kuwa Takukuru wilaya ya Kyerwa imefanikiwa kurejesha fedha kiasi cha shilingi milioni 30 zilizotolewa kwa ajili ya mkopo wa kikundi cha ufugaji nyuki cha wanawake wa Kata ya Katera ambazo ni asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri.
Alisema kikundi hicho kilipokea fedha kupitia akaunti ya kikundi namba 35910010751 iliyopo benki ya NMB tarehe 18.Februari mwaka huu baada ya kuonekana kutimiza masharti yote ya mkopo.
Alisema baada ya uchunguzi wa Takukuru ilibaini kuwa kikundi hicho kimetumika kama kikundi kivuli cha kupata mkopo husika wa milioni 30 baada ya kikundi hicho kivuli kuwekewa milioni 30 kisha zilihamishiwa kwenye akaunti namba 01J2033984900 inayomilikiwa na Benjamin Barthazari ambaye alizitumia fedha hizo kwa matumizi yake binafsi.
Alisema baada ya kubaini kasoro hizo Takukuru Kyerwa ilielekeza fedha hizo zirejeshwe kwenye halmashauri ya Kyerwa ili zitumike kama ilivyokusudiwa kwa kikundi cha wanawake .
Aidha Takukuru wamefanikiwa kudhibiti ujenzi wa chini ya kiwango wa msingi wa jengo la Zahanati ya Kijiji cha Runzenze Kata Ntobeye Wilayani Ngara inayojengwa kwa nguvu za wananchi na jumla ya shilingi milioni 9.5 kimekusanywa na wananchi wa kijiji hicho kwaajili ya ujenzi wa zahanati hiyo.
Alisema ufuatiliaji huo ulibaini kuwa kiwango cha uwiano katika mchanganyiko wa zege ( concrete ratio ) katika jamvi la msingi huo kuwa ni dhaifu kiasi cha kusababisha jamvi kuanza kumomonyoka na Nondo zilizosukwa kuonekana na kuanza kupata kutu hali inayoashiria ujenzi umefanyika chini ya kiwango.
Takukuru kwa kushirikiana na ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri, waliishauri Serikali ya Kijiji kufanya marekebisho katika hatua hiyo ya ujenzi ili kuuia madhara ambayo yangejitokeza kutokana na udhaibu wa msingi huo jamba ambalo limekwisha tekelezwa.
Alisema pia kwa kipindi cha Januari hadi Machi mwaka huu taarifa 83 zilizohusu rushwa zilichunguzwa na jumla ya majalada 12 yalifunguliwa kesi mahakamani na chunguzi zinaendelea.






