Polisi Kagera Waendesha Operesheni Maalum Kudhibiti Wizi na Madawa ya Kulevya

0


 Na Angela Sebastian 

Bukoba: Jeshi la Polisi mkoa wa Kagera limefanikiwa kukamata pikipiki 20, magari 3 na watuhumiwa 27 katika operesheni maalum iliyofanyika kuanzia mwezi Machi hadi Aprili mwaka huu, ikilenga kudhibiti wizi wa vyombo vya moto na biashara ya dawa za kulevya.

Akizungumza na waandishi wa habari leo mjini Bukoba Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Brasius Chatanda, alisema katika operesheni hiyo jumla ya watuhumiwa 18 walikamatwa wakihusishwa na wizi wa pikipiki, huku watuhumiwa wawili wakikamatwa kwa tuhuma za wizi wa magari 3 na watuhumiwa saba wakikamatwa baada ya kuuza mitumbwi mitano ya vielelezo vya uchunguzi.

Aliwataja watuhumiwa hao wa uuzwaji wa mitumbwi kuwa ni pamoja na Nicolaus  Mlaponi afisa uvuvi, John Charles afisa uvuvi, Gabriel Raphael afisa uvuvi, Isbengoma Benson, mlinzi, Elias Zacharia , mlinzi, Kennedy  Lyakurwa,  mvuvi na Wilson Rusato mkulima.

Alisema kuwa, jeshi hilo lilifanya msako pia katika operesheni hiyo lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa 101 kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo wizi wa pikipiki 20 na magari matatu,ubakaji, ulawiti pamoja na uuzaji wa dawa za kulevya.

"Tumeendelea kufanya doria mbalimbali katika ziwa Victoria na kufanikiwa  kukamata mitumbwi mitatu na watuhumiwa saba ambapo watuhumiwa hao walihusika kuuza mitumbwi mitano ambayo ilikuwa ni vielelezo vya uchunguzi wa watuhumiwa" alisema Kamanda Chatanda 

Aidha Kamanda Chatanda amesema watuhumiwa wanaendelea kushikilia ili mitumbwi miwili iliyosalia iweze kupatikana.

Katika hatua nyingine, alitoa wito kwa wananchi wa Kagera kuzingatia sheria bila shuruti ili kusaidia kupunguza vitendo vya uhalifu, hususan mauaji, ambapo amesema mkoa huo bado upo katika orodha ya mikoa 15 yenye kiwango cha juu cha matukio ya mauaji nchini na  kuwataka wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola ili kuhakikisha amani na usalama vinaimarika.




Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top