NA Ghati Msamba- Musoma
Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Pius Chaya, amesema kuwa katika kipindi cha miaka minne na nusu ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika misingi ya uchumi kwa lengo la kuvutia uwekezaji na kutatua changamoto ya ajira, hususan kwa vijana.
Naibu Waziri amesema uwekezaji huo umejikita katika sekta muhimu zikiwemo miundombinu, nishati, viwanda na huduma za kijamii, hatua ambayo imewezesha kuwepo kwa mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akizungumza katika kikao cha wadau wa uwekezaji kilichofanyika mkoani Mara, Chaya amewataka Watanzania kubadilika mtazamo na kuwa walinzi wa fursa za uwekezaji badala ya kuwa vikwazo. Amesisitiza umuhimu wa kuwekeza maarifa, nguvu kazi na rasilimali ndani na nje ya nchi kwa manufaa ya Taifa.
“Ndoto ya Taifa la viwanda na ajira kwa vijana itawezekana endapo kila wilaya itatenga maeneo yasiyo na migogoro kwa ajili ya uwekezaji na kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta matokeo chanya kwa wananchi,” amesema Chaya.
Aidha, ameeleza kuwa kuanzia sasa Taasisi ya TIZEZA ndiyo itakayokuwa msimamizi mkuu wa masuala ya uwekezaji badala ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Amesema TIZEZA itakuwa na mtandao mpana nchi nzima ili kusimamia uwekezaji kwa ukaribu zaidi na kuhakikisha manufaa yanawafikia wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Evans Mtambi, amesema Serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda, ingawa amekiri kuwa Mkoa wa Mara bado una changamoto ya ukosefu wa viwanda vikubwa.
Amesema Serikali tayari imetenga maeneo maalum kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda mkoani humo, na uwekezaji unaotarajiwa utafungua fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa uchumi wa wananchi wa Mara.
“Mkoa wa Mara una fursa nyingi za kiuchumi. Serikali imeshaandaa maeneo kwa ajili ya viwanda, hivyo uwekezaji wowote utakaokuja utakuwa chachu ya maendeleo,” amesema Mtambi.
Katika ziara yake, Naibu Waziri ametembelea Kiwanda cha Nguo cha Mute, Kiwanda cha MaziwaDaily, pamoja na Musoma Hotel, na kuielekeza Ofisi ya Msajili wa Hazina kuharakisha taratibu za kufufua viwanda vilivyokuwa vimekufa.
Pia amesema Serikali imefanya mazungumzo na Shirika la Reli Tanzania (TRC) na tayari wako katika mchakato wa kumpata mwekezaji anayetarajiwa kuanza kazi mwezi Juni mwaka huu.
Serikali imeendelea kuwasisitiza wadau wote kushirikiana kwa karibu ili kulinda uwekezaji, kuhakikisha unakuwa endelevu na unaleta tija kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa wananchi








