Na Mwandishi Wetu, Tarime.
Afisa Mwelimishaji Jamii kutoka Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na Mapambano ya Ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mara, Emmanuel Goodluck, ameshiriki Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari pamoja na Uzinduzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara kwa niaba ya Mkurugenzi wa shirika hilo, Rhobi Samwelly.
Maadhimisho hayo yalifanyika Mei 22, 2026 katika Ukumbi wa CMG uliopo mjini Tarime na kuongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mhe. Dkt. Khalfan Haule, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi. Viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na mashirika tofauti walihudhuria hafla hiyo.
Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania limeendelea kushirikiana kwa karibu na waandishi wa habari wa Mkoa wa Mara katika shughuli zake mbalimbali za kijamii. Waandishi hao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuripoti kazi za shirika hilo kwa wananchi, hasa katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia.
Miongoni mwa shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo ni kutoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia vitendo vya ukatili, pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji na ndoa za utotoni ili kuhamasisha jamii kubadilika na kuthamini haki za watoto wa kike kwa ustawi wao na Taifa pia.
Aidha, Hope for Girls and Women in Tanzania limeendelea kuthamini mchango wa vyombo vya habari na waandishi wa habari kama washirika muhimu katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kupinga mila na desturi kandamizi dhidi ya wanawake na watoto wa kike.
Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari huadhimishwa duniani kila mwaka Mei 3 kama Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari. Kwa Mkoa wa Mara, maadhimisho ya mwaka huu yamefanyika Mei 22 sambamba na hafla ya uzinduzi wa Mfuko wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara.
Mwenyekiti wa Klabu wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mara Mgini Jacob, amepongeza kazi zinazofanywa na Shirika hilo kwani zimekuwa na tija kwa Wananchi katika kuimarisha ustawi na maendeleo.



