Na; Happyness Hans WAF: Dar es Salaam
Tanzania na China zimethibitisha upya ushirikiano wao wa muda mrefu katika sekta ya afya kufuatia kukamilika kwa ujumbe wa Timu ya 27 ya Madaktari bingwa kutoka China na kuwasili rasmi kwa Timu ya 28 nchini Tanzania.
Akizungumza katika hafla hiyo Aprili 8, 2026, Jijini Dar es Salaam kwa niaba ya Waziri wa Afya, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe ameipongeza China kwa mchango wake, huku akibainisha kuwa wataalamu wa afya wa Tanzania waliopata mafunzo nchini China wameendelea kutoa mchango mkubwa kuboresha sekta ya afya.
Dkt. Seif Shekalange Ameipongeza Timu ya 27 inayoondoka kwa kuokoa maisha na kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani, huku akiikaribisha kwa moyo mkunjufu timu mpya.
Aidha,akiwakilisha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mkurugenzi wa Idara ya Asia na Australasia, Bi. Felista Rugambwa, amesisitiza msaada endelevu wa China tangu mwaka 1968, akieleza kuwa ushirikiano huo umeendelea kupanuka kutoka huduma za kitabibu hadi ujenzi wa miundombinu na uimarishaji wa uwezo wa kitaaluma kwa wataalam wa Afya.
“Ushirikiano huu unaendelea kuwa ishara imara ya urafiki wetu wa kudumu na dhamira ya pamoja ya kuboresha huduma za afya.”
Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Chen Mingjian, amesema Timu ya 28 inajumuisha wataalamu wa magonjwa ya moyo, watoto na mifupa, ambayo “wataboresha huduma za afya na faraja kwa Watanzania.” Ameongeza kuwa ushirikiano mpana umezaa matokeo makubwa, ikiwemo kuanzishwa kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kupungua kwa asilimia 70 ya magonjwa ya kichocho na malaria katika maeneo ya majaribio.
Naye Mkurugenzi wa Huduma za Tiba katika Wizara ya Afya, Hamad Nyembea, amesema mabadiliko hayo ya timu yanaimarisha uhusiano wa watu Kati ya Tanzania na China
Akitoa neno la Shukrani kwa niaba ya wenzake, Dkt. Zhang Kai amesema timu inayoondoka imehudumia wagonjwa wapatao elfu ishirini (20,000) hivi, akieleza kuwa ujumbe wao ulikuwa ni “kujenga madaraja ya urafiki.” ambapo Washiriki wa hafla hiyo walikaa kimya kwa dakika moja kumkumbuka Dkt. Zhang Junqiao, aliyekuwa mwanachama wa Timu ya 27, aliyefariki mwezi Juni mwaka 2025 alipokuwa akiokoa mwanamke aliyekuwa akizama majini.
✍️wizara ya afya







