Na Mwandishi Wetu, Arusha
Katika kukabiliana na wimbi la maudhui yasiyo na maadili yanayosambazwa mitandaoni kuhusu jamii za pembezoni, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) kwa kushirikiana na Taasisi ya Wanahabari ya kusaidia jamii za pembezoni (MAIPAC) pamoja na Idara ya Habari Maelezo, wameanza mchakato wa kuandaa mwongozo maalum utakaowaongoza wanahabari na watengeneza maudhui kufanya kazi kwa kuzingatia heshima, maadili na ridhaa ya jamii hizo.
Mwongozo huo unalenga kuweka misingi ya kitaaluma na kimaadili kwa wanahabari na watengeneza maudhui, hasa wanaposhughulikia jamii za pembezoni zikiwemo Wahadzabe, Wamasai, Wadatoga na Waakie, ambazo mara nyingi zimekuwa zikikumbwa na changamoto ya kuwasilishwa kwa namna inayodhalilisha au kupotosha uhalisia wao.
Akizungumza jijini Arusha katika mjadala wa maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani (WPFD), Mkurugenzi Mtendaji wa MAIPAC, Mussa Juma anaeleza hatua hiyo imechochewa na ongezeko la watengeneza maudhui kutoka ndani na nje ya nchi wanaoingia moja kwa moja katika jamii hizo na kurekodi au kusambaza maudhui bila kufuata taratibu wala kupata ridhaa ya wanajamii.
Anaeleza kuwa hali hiyo imekuwa ikisababisha madhara makubwa, ikiwemo kudhalilisha utu wa jamii husika pamoja na kuvunja mila na desturi zao.
“Katika siku za hivi karibuni, tumeshuhudia ongezeko la watengeneza maudhui wanaokwenda moja kwa moja katika maeneo ya jamii hizi, hususan Wahadzabe, na kutoa maudhui bila ridhaa yao, huku baadhi ya maudhui hayo yakiwa kinyume cha maadili,” anasema Juma.
Alieleza kuwa kupitia mwongozo huo, wadau wanakusudia kuweka kanuni zitakazosaidia kuhakikisha kuwa kila kazi ya uandishi au utengenezaji wa maudhui inazingatia heshima, utu na uhalisia wa jamii hizo bila kuziathiri kijamii wala kiutamaduni.
“MAIPAC kwa kushirikiana na UNESCO na Idara ya Habari Maelezo tunaandaa mwongozo maalum wa kufanya kazi katika jamii hizi kwa kuzingatia maadili na bila kudhalilisha utu wao,” amesisitiza.
Mbali na kuandaa mwongozo huo, Juma amebainisha kuwa taasisi hizo pia zina mpango wa kuzijengea uwezo jamii za pembezoni ili ziweze kutumia mitandao ya kijamii kwa manufaa yao wenyewe, ikiwemo kunufaika kiuchumi kupitia matangazo na maudhui wanayoshiriki.
Amesema kupitia ushirikiano huo, jamii hizo zitapatiwa mafunzo ya matumizi sahihi ya majukwaa ya kidijitali, pamoja na elimu kuhusu haki za kidijitali ili ziweze kujilinda dhidi ya unyonyaji wa maudhui yao.
“Tutazijengea uwezo jamii hizi kutumia mitandao kwa manufaa yao, si tu kijamii bali pia kiuchumi, kwa kutambua haki zao za kidijitali na namna ya kunufaika na maudhui yao,” aliongeza.
Katika mjadala huo, baadhi ya watengeneza maudhui mitandaoni pamoja na maafisa kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) walisisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia, ikiwemo akili unde (Artificial Intelligence), kwa njia chanya inayochochea maendeleo ya vijana na jamii kwa ujumla, badala ya kuleta madhara au kupotosha taarifa.
Wanasema pamoja na ukuaji wa kasi wa teknolojia, bado kunahitajika uwajibikaji mkubwa wa watumiaji wa majukwaa ya kidijitali ili kuhakikisha maudhui yanayozalishwa yanazingatia maadili ya kitaaluma na utu wa binadamu.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa jamii ya Wahadzabe katika eneo la Bonde la Eyasi, wilayani Karatu, Mdindi Samboga, ameipongeza MAIPAC, UNESCO, Idara ya Habari Maelezo pamoja na SAVVY Media kwa kuanzisha mpango huo ambao amesema utasaidia kurejesha heshima na manufaa kwa jamii yao.
Samboga amesema licha ya jamii yao kupata umaarufu mkubwa kwenye mitandao ya kijamii katika siku za karibuni, bado hawajanufaika ipasavyo na maudhui yanayozalishwa kuwahusu.
“Watu wanakuja wanatupiga picha na kutuhoji, tunasikia mijini tunaoneka
na sana, lakini sisi hatunufaiki zaidi ya kupewa vitu vidogo kama pombe tunaomba kusaidiwa ili na sisi tuweze kunufaika na maudhui yanayotuhusu,” amesema.
Hatua ya kuandaliwa kwa mwongozo huo inatarajiwa kuwa mkombozi kwa jamii za pembezoni, kwa kuweka mizania kati ya uhuru wa vyombo vya habari na wajibu wa kulinda utu, haki na tamaduni za jamii hizo katika zama hizi za kidijitali.





