👉Kukuza uchumi na ustawi wa wanawake na wasichana.
Na WMJJWM – Zanzibar
Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi, Zena Ahmed Said amesema ili wanawake na wasichana wastawi katika Uchumi ni muhimu kuwepo na usawa wa kijinsia katika nyanja mbalimbali za kijamii.
Balozi Zena amesema hayo leo tarehe 4 Machi katika Ukumbi wa Polisi Ziwani Mjini Zanzibar wakati wa sherehe za uzinduzi wa mradi wa PAMOJA ambao unalenga kukuza usawa wa kijinsia kwa maendeleo ya jamii.
Ndoto ya kuleta usawa wa kijinsia kupitia mradi wa PAMOJA unaotekelezwa katika Wilaya nane hapa Zanzibar ni mradi wa usawa wa kijinsia kuhakikisha kila mtu anapata fursa sawa bila vikwazo, kila mmoja wetu anastahili nafasi ya kuonesha uwezo wake” amesema Balozi Zena
Amesisitiza kwamba ni umuhimu kumuelimisha mwanamke na wasichana kwa kuwa ndiye mlezi na mwendelezaji wa kizazi cha kesho, elimu yake ni msingi wa familia imara na Taifa lenye maendeleo na kuijenga kesho iliyo bora zaidi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu ameeleza kwamba mradi huo utasaidia wanawake kupata fursa za kukuza uchumi kama mikopo yenye masharti nafuu ili kujiongezea kipato pamoja na kunufaika na elimu ya kupambana na ukatili wa kijinsia kwa ustawi na maendeleo ya jamii.
✍️maendeleo ya jamii













