Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Bw. Gerald Mweli, amekutana na kufanya mazungumzo na Uongozi wa Wakala wa Maendeleo wa Ufaransa (L' Agence Française de Développement - AFD), tarehe 25 Machi 2026, jijini Dodoma. AFD inajishughulisha na utoaji wa mikopo kwenye Sekta mbalimbali ikiwemo ya Kilimo kwa kuzingatia mazingira endelevu ili kuondoa njaa, umaskini na kuwa na usalama wa chakula kwa wakulima wadogo na lishe.
Uongozi huo umeongozwa na Bi. Celine Robert, Mkurugenzi Mkazi na Bi. Marion Vigneau, Afisa Mradi, Kilimo, Mazingira na Viumbe Hai wa AFD.
Katika mazungumzo yao, Uongozi huo umepongeza juhudi za Serikali katika kuwekeza na kuboresha Sekta ya Kilimo; huku Wizara ya Kilimo ikiombwa kushirikiana na AFD katika eneo la ufadhili wa miradi ya Sekta ya Kilimo kwenye minyororo ya thamani ya mazao ya mafuta na ngano ili kuondoa utegemezi wa kuagiza mazao hayo kutoka nje ya nchi.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Bw. Gerald Mweli amewashukuru AFD kwa kuendelea kufadhili miradi mbalimbali nchini ikiwemo Credit Guarantee Scheme (CGS) ya TADB na ameieleza AFD jinsi Serikali kupitia Wizara ya Kilimo inavyoshirikisha wadau wa Sekta Binafsi kwenye utekelezaji wa AMP 2050 ambao wamepewa kipaumbele kwenye utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 ambayo inaendana na Mpango Kabambe wa Mageuzi ya Sekta ya Kilimo 2050.
Aidha, Viongozi hao wamekubaliana AFD iendelee kutoa mitaji ya kilimo kwa ajili ya kuwezesha mikopo nafuu kupitia Taasisi za Serikali ikiwemo AGITF na TADB ambao watawafikishia wakulima kupitia CGS katika Benki za Biashara.
✍️wizara ya kilimo


