Rhobi Samwelly Atunukiwa Tuzo ya Malkia wa Nguvu 2026 Kutoka Mkoa wa Mara

0


Na Mwandishi Wetu, Musoma.

MKURUGENZI wa Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania linalojishughulisha na mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia Mkoa wa Mara Rhobi Samwelly ametunukiwa tuzo ya Malkia wa nguvu na Clouds Media group kutokana na kutambuliwa juhudi na mchango wake katika kuwasaidia Wanawake na wasichana dhidi ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia Mkoani humo.

Kupitia Shirika analoliongoza Rhobi amekuwa mstari wa mbele kupambana dhidi ya mila potofu wanazofanyiwa Watoto wa kike Mkoani humo ukiwemo ukeketaji, ndoa za utotoni na manyanyaso ya aina mbalimbali.

Ambapo ameendelea kuwapa hifadhi na kuwaendeleza kielimu ili wafikie ndoto zao. Jambo ambalo limezidi kumpa heshima kubwa ndani ya nchi na nje ya nchi na kupelekea kupewa tuzo mbalimbali kwa juhudi zake.

Rhobi amekabidhiwa tuzo hiyo Machi 25, 2026 na kampuni ya Clouds Media Group wakati wa tukio kubwa la kihistoria la kuadhimisha miaka 10 ya jukwaa la Malkia wa Nguvu, ambalo lilifanyika Serena Hotel jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa serikali, wasanii, wafanyabiashara pamoja na wanawake wenye ushawishi katika jamii.

Maadhimisho hayo ya miaka 10 yamebeba kaulimbiu ya mafanikio na mabadiliko chanya, yakionyesha safari ya jukwaa hilo tangu kuanzishwa kwake, ambapo limekuwa likiwatambua na kuwaenzi wanawake (malkia) wanaoleta mchango mkubwa katika jamii na sekta mbalimbali.

Kwa upande wake Rhobi Samwelly akizungumza na Musoma News Hub ameishukuru Clouds Media group kwa kuthamini juhudi anazozifanya katika kupambana na vitendo vya ukatili wa Kijinsia na kumtunuku tuzo hiyo.

Amesema, hatua hiyo imempa ari na molari kubwa kuendelea kuwatetea Wanawake na wasichana katika Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla katika kuhakikisha wanakuwa na ustawi bora kimaisha pamoja na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi.

"Napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa tukio hili la Malkia wa nguvu 2026. Napenda kuishukuru clouds media Group kwa kuandaa program hii ya Malkia wa nguvu na pia Kwa kuitunuku HGWT tuzo. Tuzo hii napenda kuitunuku wadau wetu wa ndani na nje ya nchi kwa kutufadhili kwa hali na mali ili kutimiza malengo ya shirika.

"Pia wafanyakazi wa shirika la HGWT, watoto wa kike na wanawake wote wanaopata huduma kutoka HGWT na Serikali yetu kwa ushirikiano mkubwa. Wizara ya Maendeleo ya jamii, Mkuu wa mkoa wa Mara, wakuu wa wilaya, Maafisa wa ustawi wa jamii, maafisa wa dawati la jinsia polisi na Maafisa wa Maendeleo ya jamii Mkoa wa Mara na Tanzania bila kuwasahau Waandishi wa habari na media mbalimbali." amesema Rhobi.



Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top