Na WMJJWM – New York, Marekani
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Mhe. Anna Athanas, amesema ni muhimu kuondoa vikwazo vinavyowazuia wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ili kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa.
Waziri Athanas ameyasema hayo wakati akifungua mjadala maalum ulioandaliwa na Chama cha Wahandisi Tanzania – Tawi la Wanawake kwa kushirikiana na Baraza la Usajili wa Wahandisi pembezoni mwa mkutano wa 70 wa Hali ya Wanawake Duniani unaoendelea jijini New York, Marekani.
Akizungumza katika mkutano huo uliohudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa mbalimbali, Waziri Athanas amesema taaluma za sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati ni msingi muhimu wa ukuaji wa uchumi, ubunifu, ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, maendeleo ya viwanda pamoja na ujenzi wa miundombinu na mifumo ya kisasa ya afya.
Ameeleza kuwa kwa mujibu wa takwimu za kimataifa, wanawake ni takribani asilimia 33 ya watafiti duniani na asilimia 35 ya wahitimu katika taaluma za sayansi na teknolojia. Hata hivyo, ushiriki wao katika fani za uhandisi na teknolojia bado ni mdogo, hali inayotokana zaidi na vikwazo vya kimfumo kuliko uwezo wa wanawake wenyewe.
Amesema kuwa Tanzania imepiga hatua katika kupanua fursa za elimu kwa wasichana, lakini bado kuna changamoto zinazowakwamisha kushiriki kikamilifu katika masomo ya sayansi hususan katika ngazi ya elimu ya sekondari, ambapo uchaguzi wa masomo kama hisabati, fizikia na kemia huamua mustakabali wa taaluma zao.
Kutokana na hali hiyo, Mhe. Anna ambainisha hatua mbalimbali za mageuzi ya sera zilizofanywa na Serikali ili kuimarisha ushiriki wa wanawake katika sekta hizo ikiwemo uhuishwaji wa Sera ya Jinsia ya mwaka 2023 inayolenga kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi kwa wanawake na kuongeza ushiriki wao katika sekta zisizo za jadi ikiwemo sayansi na uhandisi.
Aidha, ameeleza kuwa Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2023 imeweka mkazo uimarishaji elimu ya sayansi kupitia maboresho ya mitaala, matumizi ya teknolojia katika ujifunzaji pamoja na kuimarisha mafunzo ya vitendo maabara.
Amefafanua kuwa juhudi hizo zinaendana na malengo ya DIRA 2050, ambayo inaweka sayansi, teknolojia na ubunifu katika kitovu cha kujenga uchumi wa kisasa unaotegemea maarifa.
“Nipongeze juhudi zinazofanywa na Chama cha Wahandisi Tanzania – Tawi la Wanawake kwa kuanzisha klabu za sayansi mashuleni, programu za kuwafikia wanafunzi, mafunzo ya uelekezi pamoja na maonesho ya sayansi yanayowahamasisha maelfu ya wasichana kuchagua taaluma za sayansi na uhandisi.” amesema Waziri Athanas.
Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na Serikali mbalimbali, taasisi za kitaaluma, vyuo vikuu, sekta binafsi na washirika wa maendeleo ili kujenga mazingira jumuishi yanayowawezesha wanawake na wasichana kushiriki kikamilifu katika sayansi na teknolojia.
✍️maendeleo ya jamii





