Katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050 inayolenga kujenga uchumi imara na shindani, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imetoa mafunzo kwa walemavu kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti.
Mafunzo hayo yametolewa leo Alhamisi, Machi 19, 2026, wilayani Chemba mkoani Dodoma, yakihusisha walemavu wa kusikia pamoja na wasioona, kwa lengo la kuwawezesha kutambua fedha halali za Tanzania.
Akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Mawasiliano wa BoT, Afisa Mwandamizi kutoka Idara ya Mawasiliano, Bw. Sadi Makomba, amesema kuwa mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za Benki Kuu kuhakikisha kuwa hakuna kundi linaloachwa nyuma katika upatikanaji wa elimu ya fedha.
“Lengo la Benki Kuu ni kumjumuisha kila mwananchi katika elimu ya fedha, hususan makundi maalumu. Makundi haya hukumbana na changamoto ya kutambua fedha halali na hivyo kujikuta katika matatizo kutokana na ukosefu wa elimu sahihi,” amesema Bw. Makomba.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Shirika la Walemavu Mkoa wa Dodoma, Bw. Omary Lubuva, ameishukuru BoT kwa kutoa mafunzo hayo, akieleza kuwa yameziba pengo kubwa la ukosefu wa elimu ya fedha kwa kundi la walemavu wilayani Chemba.








