Na Clement Robert, WAF - Dodoma
Serikali imesisitiza kuwa na mipango madhubuti ya muda mrefu na uhakika wa upatikanaji wa dawa na vifaa tiba ili kuondoa hofu iliyojitokeza kufuatia mijadala ya kimataifa kuhusu upatikanaji wa rasilimali za afya.
Akizungumza leo Machi 26, 2026 katika Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI jijini Dodoma, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesisitiza kuwa Serikali imejipanga vyema kupitia ushirikiano wa Wizara mtambuka kuhakikisha utekelezaji wa mikakati hiyo unakuwa endelevu, akifafanua zaidi hoja ya kuwa Tanzania ina msingi imara wa kujitegemea.
Amesema pamoja na mafanikio hayo, Serikali inaendelea kuimarisha juhudi za kujitegemea zaidi katika sekta ya afya kwa kuwekeza kwenye uzalishaji wa ndani wa dawa, hatua ambayo itasaidia kupunguza utegemezi wa nje na kuhakikisha upatikanaji wa dawa unakuwa wa uhakika kwa wananchi wote.
“Tunaelekea kwenye uzalishaji wa ndani wa dawa kama mkakati wa msingi wa kuondoa utegemezi wa nje,” amesema Waziri Mchengerwa, akisisitiza dhamira ya Serikali katika kufanikisha azma hiyo ya kimkakati.
Sambamba na hilo, ameeleza kuwa Rais Dkt. Samia amemteua Bw. Emanuel Tayari kama Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia masuala ya dawa na vifaa tiba ili kuongoza juhudi za ushawishi wa uwekezaji, huku Wizara ya Afya ikitarajiwa kupatiwa eneo la Mloganzila kuanzia Aprili 1,2026 kwa ajili ya kuanzisha miradi ya viwanda vya dawa.
Aidha, Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya Bunge la afya na UKIMWI Dkt. Jonannes Lukumay amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa maono yake ya kujenga taifa linalojitegemea, akieleza kuwa uongozi wake umeweka msingi mzuri wa mageuzi ya sekta ya afya na uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini.
Amesema kamati imeridhishwa na namna ambavyo Serikali imefanikiwa kudhibiti kwa kiwango kikubwa maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto jambo linalojenga ustawi wa taifa kwa miaka mingi ijayo
Hata hivyo, juhudi hizi zinaungwa mkono na uwepo wa mazingira mazuri ya uwekezaji ambapo zaidi ya wawekezaji 40 kutoka mataifa mbalimbali ikiwemo Ujerumani na India wameonesha nia ya kuwekeza nchini.
Serikali pia inamiliki asilimia 70 ya hisa katika kiwanda cha Arusha kinachotarajiwa kuanza uzalishaji wa dawa hivi karibuni, hatua inayotarajiwa kuongeza uwezo wa ndani na kupunguza utegemezi wa kuagiza dawa kutoka nje.
✍️wizara ya afya





