Jamii yatakiwa kuacha mazoea matumizi ya dawa za kienyeji kutibu masikio kwa watoto

0


Na WAF-Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Donald Wilson Msengi ametoa wito kwa jamii na wazazi wote nchini kuacha tabia ya kutumia dawa za kienyeji kutibu masikio ya watoto na badala yake wawe mstari wa mbele katika kuwaibua watoto wenye changamoto za masikio na usikivu ili waweze kupata huduma katika vituo vya kutolea huduma za afya.

Ametoa wito huo leo Machi 03, 2026 akiwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Usikivu Duniani ambayo Kitaifa yamefanyika Mkoani Mtwara katika Viwanja vya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Kusini yakiongozwa na kauli mbiu isemayo "Kutoka Jamii Hadi Darasani: Huduma ya Usikivu kwa Watoto Wote".

"Kila mtoto katika Taifa letu ana haki ya kusikia, kusikilizwa na kustawi kwani Kauli mbiu hii inasisitiza vipaumbele viwili muhimu kama vile kuzuia upotevu wa usikivu wa watoto unaoweza kuepukika au kuzuilika pamoja na kuhakikisha utambuzi wa mapema kwani zaidi ya 60% ya upotevu wa kusikia utotoni unaweza kuzuilika” alisisitiza Kanali Msengi.

Aidha amewahimiza wazazi kutafuta usaidizi wa kitaalamu katika vituo vya kutolea huduma za Afya pindi waonapo dalili za awali za kutokwa na maji maji au  pale unapogundua mtoto ana usikivu hafifu kwani wazazi ndio watu wa kwanza kugundua mapema kuhusu maradhi ya masikio kwa mtoto hivyo waendelee kuwa karibu na watoto wao ili waweze kufuatilia ukuaji wao.

Sambamba na hilo, amewaasa wananchi kuacha imani potofu juu ya watu wenye matatizo ya usikivu kama vile uziwi unatokana na kurogwa, hautibiki, wenye changamoto hizo kutokuwa na akili hali ambayo inasababisha unyanyapaa katika jamii na kusababisha watoto kutoongea vizuri, ufaulu hafifu shuleni, kukosa kazi na kupata sonona kwa watu wazima.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Wizara ya Afya Dkt. Mwinyikondo Juma Amiri amewataka wananchi kuacha tabia ya kutumia vifaa vya kuongeza usikivu visivyozingatia ubora (earphones) na kupunguza kukaa sehemu zenye kelele nyingi ili kuendelea kulinda afya za masikio yao.

Nae Rais wa Chama Cha Wataalamu wa Masikio na Usikivu Tanzania Dkt. James Komanya amesema kuwa Maadhimisho hayo yaliambatana na kambi ya uchunguzi wa Magonjwa ya masikio na usikivu pamoja na kutoa elimu katika shule mbalimbali zilizopo Halmashauri ya Manispaa ya Mtwara Mikindani ambapo zaidi ya wananchi 4,000 wamefikiwa na huduma hizo.

Dkt. Komanya amesema kuwa mikakati ya  Chama hicho ni kuendelea kushirikiana na Wizara ya Afya kuimarisha na kurasimisha kada ya Audiolojia ili kuendelea kuimarisha huduma za usikivu kwa jamii. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi waliopata huduma za uchunguzi wa usikivu wameishukuru serikali kwa kuleta madaktari Bingwa na Bingwa bobezi ili kutoa huduma za uchunguzi na ushauri wa matibabu ya magonjwa ya Masikio na Usikivu na kwamba hatua hiyo imekuwa chachu kufahamu suluhisho la changamoto zao.

✍️wizara ya afya










Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top