Jamii imehimizwa kuendelea kuwasaidia kwa dhati watu wasiojiweza pamoja na wenye mahitaji maalum kwa kuwapatia mahitaji yao ya msingi, kuwaonesha upendo, kuwajali na kuwapa ushirikiano katika maisha ya kila siku
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara Rhobi Samwelly Machi 6, 2026.
Alitoa kauli hiyo alipokuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya siku ya Wanawake wa Wilaya ya Rorya yaliyofanyika uwanja wa Shule ya Msingi Utegi kata ya Koryo Wilayani humo.
Katika maadhimisho hayo, Rhobi alikabidhi misaada mbalimbali iliyochangwa na wadau pamoja na taasisi anayoiongoza kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum wanaosoma katika shule ya msingi Utegi.
Akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo, Rhobi aliitaka jamii kujenga utamaduni wa kusaidia watu wenye uhitaji bila ubaguzi wowote. Akihimiza kuwa, mwenyezi Mungu huwabariki wote wanaowajali wahitaji.
“Tujenge utaratibu wa kuwasaidia wahitaji katika jamii. Tunaishi na watu wenye ulemavu ambao wanahitaji kupatiwa mahitaji ya msingi. Pia wapo wengine wasio na uwezo, hivyo ni muhimu tukawajali, tuwapende na tusiwabague. Tuwape tabasamu, na kuwapa ushirikiano mzuri wanapohitaji usaidizi,” alisema Rhobi.






