Mkurugenzi wa Advocacy na Access to Justice-LHRC, Fulgence Massawe, akiwasilisha muhtasari wa tathmini ya utekelezaji wa hali ya haki za binadamu nchini Tanzania wakati wa kikao cha wadau kinachoendelea Morogoro.
Katika uwasilishaji wake, Wakili Massawe ameeleza mapendekezo yaliyotolewa kwa Serikali ya Tanzania katika mzunguko wa tatu wa UPR, akibainisha yale ambayo serikali imekubali kuyatekeleza, yale yaliyokataliwa, pamoja na yale yaliyowekwa kando kwa ajili ya uamuzi wa baadaye.
Amefafanua pia nafasi muhimu ya Asasi za Kiraia katika mchakato wa UPR, akisisitiza wajibu wao katika kufuatilia utekelezaji wa mapendekezo yaliyokubaliwa na serikali pamoja na kushiriki katika maandalizi ya Shadow Report, ambayo ni ripoti huru ya wadau inayowasilishwa kimataifa kama sehemu ya mchakato wa tathmini.
Massawe amebainisha kuwa maandalizi ya ripoti hiyo yanafuata taratibu na muda maalum wa kimataifa ili kuhakikisha taarifa za wadau zinawasilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vinavyotakiwa.
Aidha, ameangazia baadhi ya masuala muhimu yaliyopewa kipaumbele katika rasimu ya ripoti ya wadau wa UPR, ikiwemo umuhimu wa kulinda na kuimarisha nafasi ya kiraia (civic space) ili kuhakikisha uhuru wa kujieleza na kukusanyika unaheshimiwa huku akisisitiza umuhimu wa serikali kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali na bajeti ya kutosha kwa ajili ya kutekeleza mipango ya kitaifa inayolenga kulinda na kukuza haki za binadamu.
Uwasilishaji huo umetoa muhtasari mpana wa ahadi za Tanzania katika mfumo wa UPR, hali ya utekelezaji wake pamoja na nafasi ya wadau mbalimbali katika kufanikisha mchakato huo.
✍️ Legal and Human Rights Centre





