Mkurugenzi wa Save the Children Tanzania, Angela Kauleni, ameeleza umuhimu wa kulinda haki za watoto na kuhakikisha wanakua katika mazingira salama, yenye upendo na yanayowapa nafasi ya kukua kama binadamu wenye thamani, wakati akihutubia kikao cha wadau cha uhakiki wa ripoti ya Asasi za Kiraia kwa mzunguko wa nne wa Universal Periodic Review (UPR) Morogoro.
Kauleni amefafanua kuwa zaidi ya nusu ya Watanzania ni watoto, na ingawa hawana uwakilishi rasmi katika maamuzi ya taifa, kila uamuzi unaofanywa leo unaathiri kesho yao. UPR ni fursa ya kuhakikisha sauti za watoto, mahitaji, ndoto na changamoto zao, zinaingizwa katika mjadala wa kitaifa na kimataifa na kufanyiwa kazi.
Amesisitiza mafanikio ya Tanzania katika kulinda haki za watoto, ikiwemo kupungua kwa ukatili dhidi ya watoto kwa 26.5%, kuimarika kwa usajili wa vizazi, mwongozo unaowawezesha wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni, na uimarishaji wa huduma za kijamii.
Pamoja na hayo, Kauleni amebainisha changamoto zinazohitaji mwitikio wa pamoja: uhaba wa maafisa wa ustawi wa jamii, sheria zilizopitwa na wakati, changamoto za watoto wenye ulemavu, ajira hatarishi, ukatili wa kimtandao na madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Amesisitiza kuwa mkutano wa leo si wa kukagua ripoti tu, bali ni fursa ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na Asasi za Kiraia, na kuhakikisha ajenda za watoto zinawekwa katikati ya mchakato.
Kauleni amehitimisha kwa kusema kuwa kizazi cha sasa kinayo jukumu la kuhakikisha kila mtoto anapata nafasi ya kukua kwa usalama, heshima na matumaini. Mtoto anayelelewa salama leo ndiye kiongozi, raia mwadilifu na nguvu ya uchumi wa kesho wa taifa. Amesema kuwa kwa ushirikiano wa wadau, Tanzania inaweza kujengwa kwa watoto ambao ni salama, wanafurahia utoto wao, wanapata elimu bora, na wanafikia ndoto zao bila vikwazo.
✍️Legal and Human Rights Centre


