Wananchi Dar es Salaam Wapongeza Huduma za Kliniki ya Sheria

0



Wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam wameendelea kujitokeza na kueleza kuridhishwa na huduma za ushauri wa kisheria bila malipo zinazotolewa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Kliniki ya Sheria bila malipo kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam inayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza kuhusiana na  mwitikio wa wananchi katika  Kliniki ya Sheria, Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri wa Kisheria ya mkoa wa Dar es Salaam na Wakili wa Serikali wa Mkoa Bi. Mwema Punzi amesema kuwa mwitikio  wa wananchi ni mkubwa, jambo linaloonyesha kiu ya wananchi kupata uelewa wa sheria.  

*“Wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi kupata huduma mbalimbali za kisheria, hii inatupa picha kuwa uhitaji wa huduma za kisheria kwa wananchi ni mkubwa.”* Amesema Bi. Mwema 

Katika hatua nyingine, Wakili wa Serikali Mkoa wa Dar es Salaam ametoa rai kwa wananchi wa mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kutembelea Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini Dar es Salaam kupata huduma mbalimbali za kisheria.

*“Tunawasisitiza wananchi waendelee kutembelea katika viwanja hivi wapate huduma zetu, tuna timu ya Mawakili wa Serikali  hapa wako tayari kutatua changamoto mbalimbali za ksiheria zinazowakabili wananchi.”* Amesema Bi. Mwema 

Kwa upande wao, Wananchi waliofika katika kliniki hiyo wameonekana kufurahishwa zaidi na weledi na lugha rafiki inayotumiwa na Mawakili wa Serikali wanaotoa huduma ya ushauri wa kisheria. 

Bw. Husein Mfaume mkazi wa Ilala Jijini Dar es Salaam, ametoa pongezi kwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuendesha Kliniki ya Sheria bila malipo kwakuwa itasaidia kutatua changamoto na migogoro ya kisheria hususan kwa wananchi wenye kipato cha chini.

*Nina la suala la mirathi lilinisumbua kwa muda mrefu bila kujua hatua za kuchukua, kupiti kliniki hii nimekutana na Mawakili wa Serikali wamenipa mwanga na nimejua haki yangu. Hii kliniki ni mkombozi kwetu sisi wanyonge."* Amesema Bw. Husein.

Kwa upande wake Bi. Diana Chilowaka ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuifanya Kliniki hiyo Jijini Dar es Salaam, ambapo kupitia Kliniki hiyo wananchi wameweza kupata huduma za kisheria bila malipo, pia ameiomba Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kufanya Kliniki hizo mara kwa mara ili kuwafikia wananchi wengi zaidi.

*“Niwapongeze Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuja kutoa huduma hii bure, Mawakili, wnaatusikiliza kwa upole na kutupa ushauri bila kututoza hata shilingi moja. Tunaomba huduma hizi ziwe endelevu."* Amesema Bi. Diana

Kliniki ya Sheria bila malipo ilizinduliwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila tarehe 16 Februari, 2026 na inaendelea hadi tarehe 22 Februari, 2026 katika Viwanja vya Mnazi Mmoja Jijini, Dar es Salaam.

✍️ofisi ya mwanasheria mkuu


Chapisha Maoni

0 Maoni
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
Chapisha Maoni (0)

#buttons=(Accept !) #days=(20)

Our website uses cookies to enhance your experience. Learn More
Accept !
To Top