Na Oscar Tarimo WMJWM Arusha
Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kusimamia na kuimarisha jitihada kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa kama msingi wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa jamii na uchumi jumuishi.
Wakili Amon Mpanju ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya uandaaji na uwasilishaji wa Habari zenye uchechemuzi wa masuala ya Jinsia tarehe 23, februari, 2026 jijini Arusha.
Wakili Mpanju amesema Serikali inaamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana endapo sehemu ya jamii itaachwa bila kushiriki katika fursa zilizopo kwenye jamii ili kuondokana na mifumo ya ubaguzi na ukosefu wa haki unaotokana na jinsia.
Wakili Mpanju ameongeza kuwa usawa wa kijinsia siyo suala la wanawake pekee, bali ni ajenda ya kitaifa inayolenga kujenga jamii yenye haki, heshima, ushirikiano na maendeleo kwa wote hivyo mafunzo hayo yanasaidia kuleta uelewa kuwa usawa wa kijinsia hauondoi nafasi ya mwanaume katika jamii, bali kujenga jamii yenye uwiano, haki, na maendeleo kwa wote.
”Haya ni mafunzo ya kipekee na kimkakati kwa sababu yanawakutanisha waandishi wa habari ambao ni sauti ya jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ambao ni nguzo ya ulinzi na ustawi wa watu, watendaji wa kata ambao ni kiungo cha Serikali na wananchi, pamoja na maafisa utumishi ambao wana jukumu la kusimamia mifumo ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu kwa misingi ya haki na usawa.” amesema Wakili Mpanju
Amesitiza kuwa mafunzo hayo masuala ya usawa wa kijinsia yamekuja ikiwa ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosisitiza kuwepo na usawa kwa watu wote pamoja na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa iliyokubakiwa nchini ambayo inayosisitiza uwepo wa usawa wa kijinsia.
“Tunapopinga ubaguzi wa kijinsia, tunalenga kuondoa mifumo inayomnyima mwanamke au mwanaume fursa kwa misingi ya jinsia. Kwa hiyo, jumbe zetu lazima ziwe jumuishi.
✍️maendeleo ya jamii









