Na Jackline Minja WMJJWM, Dodoma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, amesema Serikali imeanza rasmi hatua muhimu ya kuhakikisha bajeti zote zinaandaliwa kwa kuzingatia usawa wa kijinsia ili kukidhi mahitaji ya makundi yote ya jamii bila ubaguzi.
Akifungua mafunzo ya uandaaji wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia yaliyofanyika Februari 17, 2026 katika Ukumbi wa St. Gasper jijini Dodoma, Mdemu amesema mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa Mwongozo wa Bajeti wa mwaka wa fedha 2026/2027 unaolenga kuimarisha ujumuishi katika mipango na matumizi ya rasilimali za umma.
“Mafunzo haya ni hatua muhimu katika utekelezaji wa Mwongozo wa Bajeti wa mwaka wa fedha 2026/2027 unaoelekeza Serikali kuanza rasmi mchakato wa uandaaji wa bajeti yenye mrengo wa kijinsia, hatua hii inalenga kuhakikisha mipango na bajeti za Serikali zinazingatia mahitaji ya makundi yote ya jamii wakiwemo wanawake, wanaume, vijana, watoto na watu wenye ulemavu,” amesema Mdemu.
Ameongeza kuwa Serikali imeanza utekelezaji huo kwa majaribio katika Wizara tisa ambazo ni Kilimo, Elimu, Katiba na Sheria, Maji, Afya, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mifugo na Uvuvi, Viwanda na Biashara pamoja na Mambo ya Ndani, huku mikoa ya Geita na Singida na Halmashauri za Tandahimba pamoja na Chalinze.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru, amesema mafunzo hayo yanalenga kujenga uwezo wa watendaji kutoka sekta mbalimbali ili waweze kutekeleza kwa vitendo dhana ya bajeti yenye mrengo wa kijinsia na kuwasisitiza washiriki kuzingatia mafunzo hayo kwa umakini ili yaweze kuleta matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha usawa wa kijinsia kupitia mifumo ya mipango na bajeti, hatua inayotarajiwa kusaidia kupunguza pengo la kijinsia na kuleta maendeleo endelevu nchini.
✍️maendeleo ya jamii









