Na Mwandishi Wetu.
WANANCHI wametakiwa kuendelea kuwafichua mbele ya vyombo vya sheria wanaofanya vitendo vya ukatili wa kijinsia bila kuwafumbia macho, hatua ambayo itasaidia kutokomeza vitendo hivyo na kuimarisha ustawi bora katika jamii.
Wito huo umetolewa Februari 17, 2026 na Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Kiserikali la Hope for Girls and Women in Tanzania (HGWT) linalojishughulisha na mapambano ya ukatili wa kijinsia mkoani Mara, Rhobi Samwelly, wakati akitoa elimu ya ukatili kwa baadhi ya wananchi wa Wilaya ya Butiama.
“Ndugu zangu, Serikali na wadau tunaendelea kupigia kelele vitendo vya ukatili wa kijinsia. Ili kuvitokomeza, wafichueni wanaofanya ukatili bila kuwafumbia macho. Toeni taarifa mapema polisi, Serikali za mitaa, katika Madawati ya Jinsia, ama sehemu ambazo hatua zitachukuliwa haraka. Wanaofanya ukatili wakati mwingine ni watu wa karibu, msiogope kuwataja,” amesema na kuongeza kuwa:
“Tunatambua kwamba ukeketaji na ndoa za utotoni havikubaliki kisheria. Mkiona kuna mtu anaandaa mpango wa kumkeketa mtoto wake wa kike, toeni taarifa mapema ili kabla ukatili huo haujafanyika mhusika achukuliwe hatua haraka. Pia, ukatili mwingine mkiona unataka kufanywa na mwanajamii, chukueni hatua mapema. Lengo ni kuhakikisha tunatokomeza ukatili na tunaendelea kujenga jamii imara,” alisema Rhobi.
Aidha, amewataka wananchi kuweka mkazo katika kuwasomesha watoto wa jinsi zote, ambapo amesema elimu ndiyo urithi pekee utakaoendeleza kizazi cha watu wasomi ambao ni tegemeo katika kuleta mageuzi chanya katika jamii na Taifa pia.
Jesca Marwa, ambaye ni mkazi wa Kiabakari Wilaya ya Butiama, amesema jamii inapaswa kuendelea kuelimishwa kuhusu madhara ya vitendo vya ukatili. Pia amelipongeza Shirika hilo kwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili kusaidia kuleta mabadiliko kwa wananchi.
Kwa upande wake, Daud Warioba amesema moja ya sababu inayochangia vitendo vya ukatili kuendelea kwenye jamii ni matukio hayo kumalizwa kwa njia ya mazungumzo baina ya muathirika na mhusika aliyefanya tukio. Ameongeza kuwa, ili kuvitokomeza, ni lazima njia za kisheria zitumike.


