Dar es Salaam : Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dkt. Diwani Msemo, amesema msaada uliotolewa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) wa zaidi ya Sh. Milioni 361.5 kukarabati chumba cha upasuaji na uwekaji vifaa tiba utaleta furaha kwa wananchi.
Ameyasema hayo wakati akipokea msaada huo uliokabidhiwa na Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama (PSSSF), Bw. Omega Ngole, kwaniaba ya Mkurugenzi Mkuu Bw. Fortunatus Magambo, katika hafla iliyofanyika kwenye taasisi hiyo jijini Dar es Salaam, Februari 23, 2026.
“ Mlichofanya leo hii kimekuja kuleta majibu ya miaka 30 iliyopita, chumba hiki cha upasuaji kilitakiwa kuwepo tangu mwaka 1996, tunashukuru kwa kuungana na serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kupeleka furaha kwa wananchi,” alisema Dkt. Msemo.
Alisema, msaada huo unagusa moja kwa moja maisha ya wananchi kwa kuwa na chumba cha kisasa cha upasuaji kwa wagonjwa wa saratani lakini pia vifaa vyake.
“ Tunaimani kwamba tutakuwa tumewekeza kwa watanzania lakini pia na wastaafu wetu kwasababu watahitaji hizi huduma.” Alisisitiza Dkt. Msemo.
Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Elimu kwa Wanachama, Bw. Omega Ngole, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu, alisema, uamuzi wa kutoa kiasi hicho cha fedha ulitokana na ziara ya awali iliyobaini kuwa taasisi hiyo haina chumba cha upasuaji kinachojitegemea kwa ajili ya wagonjwa wa saratani.
Akifafanua kuhusu msaada huo, Bw. Ngole alisema, Sh. Milioni 197,027,956 zitatumika kukarabati chumba cha upasuaji wa saratani na Sh. Milioni 164,491,270 zitatumika kununulia vifaa tiba kwa ajili ya chumba hicho.
" PSSSF inajisikia faraja kuunga mkono jitihada za serikali katika hospitali hii na sekta ya afya kwa ujumla, Mfuko unahudumia wananchi na ni vizuri pia kutowasahau wananchi ambao wengine ni wanachama wetu.” Alisema na kuongeza, msaada huo kupitia sera ya PSSSF ya uwekezaji kwa jamii maarufu kama CSI chini ya kaulimbiu ya #PSSSFKaribunaJamii, watanzania wengi wakiwemo wanachama wa PSSSF watafaidika.
✍️Psssf









